Historia ya ujenzi wa Tazara itusute, tuitunze

JANA nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari wa kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN) ambao tulikwenda kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing ambaye alikuwa anazungumzia ziara ya waziri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi.

Mwisho wa mazungumzo yetu mmoja wa wasaidizi wake alitukabidhi vitabu, kimoja kinaitwa Xi Jinping; The Governance of China na kingine ni A Monument to China- Africa Friendship.

“Nendeni mkasome vitabu hivi, ni vizuri na vitawasaidia katika kazi zetu mtakapokuwa mnaandika habari zozote kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na China,” alisema Gou Haodong ambaye ni ofisa katika ubalozini hapo.

Ni vitabu vikubwa, lakini wakati niko njiani kurudi ofisini nilichagua kuanza kusoma kitabu cha A Monument to China -Africa Friendship na katika ukurasa wake wa kwanza tu mada wanayozungumzia ni ujenzi wa reli ya Tazara.

Katika ukurasa huo, kichwa cha habari kinasomeka, mazingira yaliyofanya China ikubali kusaidia ujenzi wa reli ya Tazara na aliyehojiwa ni Zhou Nan ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China wakati huo.

Katika mada hiyo, waziri huyo ameelezea namna ambavyo China ilijihusisha na siasa za Afrika miaka 1960 wakati huo nchi nyingi zikiwa zinapigania uhuru na katika eneo hili la Afrika ilikuwa ni Ghana pekee ambayo ilikuwa imepata uhuru.

Pia ameelezea namna ambavyo Tanganyika ilipata uhuru na kuwa nchi ya kwanza katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata uhuru chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere. Lakini pia mwandishi akaelezea namna China ilivyojishughulisha na siasa za Afrika kwa kuamini kuwa ndio wanaweza kuwa marafiki wao wa dhati.

Lakini kilichonivutia zaidi ni kwamba China ilikuja kukubali kujenga reli ya Tazara baada ya kuombwa na Mwalimu Nyerere kwa lengo la kuinua uchumi wa Tanzania na Zambia, lakini pia kwa lengo la kusaidia ukombozi wa kisiasa kwa nchi ambazo zilikuwa hazijapata uhuru wake.

Msimuliaji anasema wakati wa kusaka fedha za kujenga reli hiyo, Mwalimu Nyerere alianzia kuziomba nchi za magharibi zisaidie fedha za ujenzi huo, lakini zilikataa, akaenda Urusi pia haikuwa tayari kutoa fedha hizo na ndipo alipokwenda kwa China.

“Nyerere alimtuma waziri wake wa Biashara Abdulrahman Babu kwenda kuzuru China mwaka 1965 ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa China. Ndipo alipopeleka ujumbe wa Nyerere kwa Serikali ya China kwamba Rais Nyerere anataka kujenga reli, lakini kwa kuwa hakuna ambaye yuko tayari kumsaidia kwa nchi za Magharibi na Urusi, anakuja kwenu China ili msaidie,” inasema sehemu ya kitabu hicho.

Kitabu hicho kinasema wakati Nyerere anawasilisha maombi hayo, China ilikuwa imepatwa kwenye majanga ya asili na hivyo ilikuwa na hali mbaya ya kiuchumi na watu wake walikuwa wanaishi maisha magumu. Waziri huyo anasema, Babu wakati anawasilisha ombi hilo alijua hali ngumu ya kiuchumi iliyokuwepo, lakini aliisihi China isikatae ombi hilo badala yake ikae ifikiirie.

“Mkikataa ombi letu mtakuwa mmemkatisha tamaa Mwalimu Nyerere.” Baada ya kutafakari kwa kina Serikali ya China ambayo wakatia huo ilikuwa na viongozi ambao ni Mao, Liyu Shaoqi na Zhou Enlai hakuwa na namna zaidi ya kusema ndiyo tutakwenda kujenga reli kuunganisha nchi za Tanzania na Zambia.

Kiukweli sipaswi kuendelea kuzungumzia yaliyoko kwenye kitabu hicho, kwa sababu nafasi haitoshi, ila ninachoweza kusema tu ni kwamba Tazara kwa China ni alama muhimu sana ya uhusiano uliopo baina ya nchi hizi mbili. Ni uwekezaji walioufanya wachina wakati wana hali ngumu ya uchumi.

Walifanya hivyo kwa kuamini tu kuwa walikuwa wanawasaidia ndugu zao ili waweze kuinuka kiuchumi, lakini pia waweze kuzikomboa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.

Ninasikitika ninapoona alama hii mojawapo ya urafiki wa kweli kati ya Tanzania na China tumeshindwa kuitunza, kuiendeleza na sasa iko taabani. Hii ni aibu kubwa kwa Tanzania na Zambia, ni lazima tutunze uwekezaji huu, kwani bado ni muhimu kiuchumi kwa nchi zetu. Udumu urafiki wa China na Tanzania.