Chaneta ihamasishe maendeleo mchezo wa Netiboli nchini

HIVI karibuni yalifanyika mashindano ya taifa ya mchezo wa netiboli mkoani Dodoma, ambapo timu ya netiboli ya Mkoa wa Morogoro iliibuka na ubingwa wa mashindano hayo.

Katika mashindano hayo ni mikoa mitano tu ambayo ni Dodoma, Mwanza, Manyara, Morogoro na Kinondoni (mkoa kwa mujibu wa mchezo wa Netiboli) ambayo ilipeleka timu kwenye mashindano hayo. Ushiriki wa timu chache za mikoa katika nchi yenye mikoa zaidi ya 20 inaashiria kuwa mikoa mingine imezembea kujitokeza kwenye mashindano hayo ya kitaifa.

Kujitokeza kwa mikoa michache kwenye mashindano ni dhahiri kuwa inapunguza radha ya mashindano hayo ambayo yangetakiwa kuwa makubwa na yenye msisimko. Lakini kwa kujitokeza kwa mikoa michache kuwakilisha kwenye mashindano hayo ni dhahiri kuwa kwa sasa kunatakiwa kuwapo kwa mkakati madhubuti wa kuhamasisha mchezo huo.

Iwapo kama Chama cha Mchezo wa Netiboli Tanzania (CHANETA) kikiwa na mkakati mathubuti wa kuhamasisha maendeleo ya mchezo huo, utakuwa na mvuto hali itakayoongeza ushiriki wa timu nyingi kwenye mashindano.

Ni wazi kuwa kwa sasa hakuna hamasa kubwa ya mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo kila kulipokuwa na michuano mikubwa kama hiyo ya kitaifa timu nyingi zilikuwa zikijitokeza. Kama kukiwa na hamasa kubwa na ushiriki wa timu ukaongezeka ni wazi kuwa kutakuwa na wadhamini watakaojitokeza kuongeza nguvu kwenye mashindano hayo.

Hamasa inatakiwa kuanza tangia kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka kupitia katika shule mbalimbali za sekondari pamoja na vyuo. Hamasa ikianzia kwenye shule na vyuo inasaidia kwa kiasi kikubwa kuwavutia wanafunzi kuwa karibu na mchezo huo na kuushiriki.

Kama Chaneta ikifanikiwa kuwa na timu za shule na vyuo kushiriki michuano hiyo itasaidia kukuza mchezo huo kwa kuwa huko ndipo kwenye nguvu kubwa ya vijana. Kama Chaneta ikijipanga inaweza kupata kampuni ya kuingia nayo makubaliano ya udhamini iwe ya simu au nyinginezo zozote kwa kuwa Netiboli ni moja kati ya michezo mikubwa nchini.

Kwa kuwa kuna kalenda ya mashindano kuanzia ngazi za wilaya, mkoa, Ligi Daraja la Kwanza pamoja na ya kitaifa basi Chaneta ianze sasa kutafuta wadhamini ambao watadhamini mchezo huo.

Lakini hiyo ni lazima iende sambamba na hamasa ya vyombo vya habari katika kuyatangaza mashindano hayo katika vyombo iwe Radio, Luninga, Magazeti na hata kwenye yale magazeti tando (blogs).

Hivyo basi ni jukumu letu pia kwa waandishi wa habari kuendelea kuunga mkono jitihada zitakazoanzishwa na Chaneta katika kuleta hamasa mpya ya mchezo huo. Kwa pamoja wanahabari kwa kushirikiana na Chaneta tunaweza kuuendelea mchezo huo na kuufanya kuwa moja kati ya michezo mikubwa yenye kuwavutia vijana wengi nchini.