Upungufu wa wauguzi Dar ufanyiwe kazi

JANA katika gazeti hili kulikuwa na habari iliyokuwa ikisema ‘Upungufu wa wauguzi wawa tishio Dar’. Habari hiyo ilikuwa ikionesha upungufu wa wauguzi hao na kwamba kwa sasa ni ni tatizo kubwa, kwa kuwa waliopo hawatoshelezi.

Idadi ya ya wauguzi walioko katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam ni ndogo mno, ikilinganishwa na wagonjwa wanaowahudumia kila siku, hali inayochangia huduma mbovu katika hospitali hizo. Suala la kuwa na afya bora ni muhimu kwa kila mmoja wetu na hasa kwa kuzingatia hakuna maendeleo bila kuwa na afya bora.

Katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchumi wa viwanda, Watanzania wanatakiwa kuwa na afya bora, kwa kuwa ndio nguvu kazi itakayoshiriki katika viwanda vitakavyoanzishwa. Katika mkoa wa Dar es Salaam inaelezwa kuna upungufu wa wauguzi kwa asilimia 42 ili kufikia mahitaji halisi, kwani kwa sasa mkoa huo una wauguzi zaidi ya 2,181 ambao ni pungufu.

Upungufu huo wa wauguzi hauendani na uwiano unaokubalika na Shirika la Afya Duniani (WHO), ambao unaelekeza kuwa muuguzi mmoja mwenye stashahada, shahada ya uzamili na uzamivu anapaswa kuhudumia wagonjwa kati ya nane hadi 10 na mwenye cheti anapaswa kuhudumia wagonjwa wanne hadi sita.

Kutokana na uchache huo wa wauguzi, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wanaodai kuwa huduma ni mbovu, hivyo kutaka ziboreshwe ili kuwa na jamii yenye afya bora. Japo tatizo la uhaba wa watumishi wa sekta ya afya ni tatizo ambalo lipo karibu nchini, lakini kuna haja ya kuangalia namna ya kuongeza wauguzi ili kama si kumaliza, basi kupunguza sehemu kubwa ya uhaba huo.

Uwezekano wa kutoa huduma ambazo ni mbovu kwa wagonjwa kutokana na ukweli kwamba wauguzi hao huzidiwa na wagonjwa, kwani kwa sasa muuguzi mmoja huhudumia wagonjwa zaidi ya 20 kwa siku na wakati mwingine wagonjwa wa wodi zima.

Kwa mujibu wa Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ziada Sellah, uhaba wa wauguzi katika mkoa huo ni kubwa, ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa wanaopokelewa kwa siku na idadi hiyo kutolingana na fedha iliyotengwa, hali inayosababisha upungufu wa vifaa tiba, dawa na watumishi.

Sellah anasema watumishi wa hospitali za manispaa zilizopo Dar es Salaam na idadi yao kwenye mabano ni Ilala (721), Kinondoni (605), Kigamboni (162), Temeke (474) na Ubungo (219), ambayo haitoleshi mahitaji halisi ya mkoa huo.

Lakini, pia wananchi nao tunapaswa kushiriki katika kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa, kwa kupaza sauti zetu pale tunapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, kulipa kodi ili kodi hizo zitumike kuboresha hospitali zetu na pia kuchangia pale tunapotakoiwa kufanya hivyo.

Pamoja na kwamba wananchi hatuwezi kuwaajiri watumishi hao, lakini ushiriki wetu utaweza kuipa nguvu serikali ya kuajiri na kuongeza watumishi na wauguzi hao wa afya katika hospitali zetu na hatimaye kufika malengo na uwiano wa WHO. Naamini Watanzania watakuwa wakiipongeza serikali katika juhudi zake za kuboresha huduma za afya.

Hivyo na hili la wauguzi, naamini pia Serikali italiona na kuangalia namna ya kutatua changamoto hiyo ya upungufu wa wauguzi katika hospitali za jiji la Dar es Salaam pamoja na hospitali mbalimbali nchini.

Pia ni imani yangu kuwa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, inatambua tatizo hilo na unalifanyia kazi ili wananchi wake wawe ni wenye wenye afya bora na kuweza kupeleka mbele gurudumu la maendeleo kuelekea uchumi wa kati.