Walimu kutozwa fedha za vitambulisho ni uonevu

MOJA ya habari iliyopo kwenye gazeti hili ni pamoja na walimu wa shule za msingi na sekondari kuchangishwa fedha za kutengeneza vitambulisho na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Karatu.

Katika taarifa hiyo, imebainisha kuwa watumishi hao wamediriki kuwatoza walimu hao kiasi cha Sh 6,000 ili waweze kupata vitambulisho vyao vya utumishi, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kazi.

Kwa mujibu wa taratibu za kazi, kila mtumishi anastahili kupatiwa kitambulisho chake cha kazi na mwajiri kwa gharama za mwajiri husika kwani mwisho wa siku kitambulisho husika huwa ni mali ya mwajiri.

Hivyo basi kitendo cha watumishi hao wa halmashauri ya wilaya ya Karatu kuwatoza fedha walimu ili wapatiwe vitambulisho kinapaswa kuchunguzwa ili kuweza kubaini fedha hizo zinakwenda wapi.

Ni aibu na fedheha kwa watumishi wa halmashauri hiyo kuwachangisha fedha walimu wa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya kuwatengenezea vitambulisho vya kazi.

Aibu hii haipaswi kuvumiliwa na inatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa watumishi hao waliokusanya fedha hizo. Kwa mujibu wa taarifa iliyopo ni kwamba pamoja na walimu kutozwa fedha hizo wapo waliopatiwa vitambulisho na wengine hadi sasa wanaendelea kusubiri.

Mamlaka husika zinapaswa kufuatilia kwa makini suala hili, kwani uonevu wa watumishi hususani walimu kama hao, unapaswa kuchukulia hatua za kinidhamu ili kutoa fundisho kwa waonevu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Theresia Mahongo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Waziri Morice kwa pamoja wanapaswa kufuatilia kwa kina ni nani aliyechukua fedha za walimu hao wengi na alizipeleka wapi.

Sote tunajua umuhimu wa walimu hakuna mtu yeyote yule ambaye hajafundishwa na walimu hao hadi hapo walipofikia na kujikwamua kimaisha sasa, iweje walimu hao hao wanaofundisha watoto wetu wadhulumiwe haki zao huku wengine wakinufaika kwa hela za wenzao.

Pia mwalimu huyo unayechukua hela zake yeye ndio ufunguo wa maarifa kwako wewe na wengine na bado anadai fedha zake za kupandishwa madaraja, nauli na nyingine, hivi hata fomu ya opras nazo mnataka atoe nakala kwa hela yake mwenyewe ili ajaze wakati anastahili kupewa fomu hizo na kuzijaza bila usumbufu.

Naomba tuwe na huruma kwa walimu na nyie mnaotoa huduma kwa watumishi wenzenu acheni kuwanyanyasa kwa kudai haki zao hivi kweli hata vitambulisho vya kazi mtumishi anakatwa hela yake wakati anapaswa kupewa bure?

Nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa kuongea na walimu hao na kubaini changamoto hiyo sambamba na kuwapa moyo kuendelea kufundisha wanafunzi huku serikali ya Mkoa wa Arusha ikifuatilia kwa karibu jinsi ya kupata fedha kwa ajili ya kulipa baadhi ya madeni ya walimu katika wilaya zote za mkoa wa Arusha.