Dar es Salaam mjitathmini upya katika mfumo wa elimu

JUZI Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) lilitangaza matokeo ya Kidato cha Nne kwa mwaka 2016 na kuonesha kwamba ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.44.

Matokeo hayo pia yameonesha kwamba watahiniwa wa shule 244,762 ambayo ni sawa na asilimia 70.35 ya waliofanya mtihani walifaulu mtihani huo. Pamoja na matokeo hayo kuonesha kwamba ufaulu umeongezeka, lakini Mkoa wa Dar es Salaam umeonesha kuzorota kielimu baada ya kuwa na shule sita kati ya 10 zilizoshika nafasi za mwisho.

Shule hizo ni pamoja na shule ya Sekondari Kitonga, Nyeburu, Mbopo, Mbondole, Somangila Day na Kidete. Shule zingine ni Masaki (Pwani), Dahani (Kilimanjaro), Ruponda (Lindi) na Makiba (Arusha).

Kutokana na hali halisi ya uchumi na mazingira ni wazi kwamba watu wengi walitarajia kwamba mkoa wa Dar es Salaam ambao ndilo jiji kubwa ungekuwa unaongoza kwa shule zenye matokeo mazuri kutokana na miundombinu yake pamoja na fursa nyingi za kujisomea zilizopo.

Ni kweli kwamba majiji au miji huwa ina miundombinu mingi ambayo huwezesha mazingira yoyote ya kielimu hata kibiashara kufikiwa kwa urahisi. Tunategemea kwamba kwa vile mkoa wa Dar es Salaam una huduma nyingi za kielimu ikiwemo maktaba, maabara, walimu wa kutosha na nyenzo za kufundishia shule zake na wanafunzi wake walipaswa kung’ara katika matokeo na kuwa mfano kwa shule nyingine.

Sote tunafahamu kwamba mjini zinapatikana huduma nyingi nzuri ambazo zinatoa fursa kwa wanafunzi kupata muda na vifaa vingi zaidi vya kujifunzia ikilinganishwa na maeneo ya vijijini ambao kwao hata kupata vifaa vya maabara kwa ajili ya kujifunzia huwa ni tatizo.

Mbali na huduma pia shule nyingi za mjini zina walimu wengi ikilinganishwa na shule za vijijini, hivyo inatia shaka kuona shule ambazo zenye huduma wanafunzi wake wanapata matokeo mabaya au zinashika mkia.

Kwa mazingira ya mijini tunafahamu pia wanafunzi wengi wanapata nafasi ya kujisomea ikilinganishwa na maeneo ya vijijini ambapo mwanafunzi hutumia muda mwingi kufika nyumbani kutokana na umbali wa shule na baada ya kufika nyumbani hujikuta akiwa majukumu mengi ya kusaidia shughuli za nyumbani zikiwemo hata kutafuta chakula kabla ya kupata muda wa kujisomea.

Kutokana na haya ni wazi kwamba shule nyingi za mjini wanafunzi wake wanapaswa kuongoza na si kuwa mkia kama ilivyotokea kwa Dar es Salaam. Kwa maana hiyo, ipo haja kwao wanaohusika kujiangalia na kujitathmini ili kuona ni wapi wameteleza ili kuhakikisha wanarejesha heshima ya elimu bora katika mkoa huo.

Inasikitisha kuona mkoa huo ambao unaaminika kwa mengi ndiyo unatoa shule sita zilizofanya vibaya kati ya 10. Kwa hili inapaswa kufanyika jitihada za makusudi ikiwemo mamlaka za elimu na mkoa husika kuhakikisha wanazitembelea shule hizo mara kwa mara ili kujua changamoto zake na kuangalia namna ya kuzitatua ili kuondoa taswira hiyo mbaya iliyojengeka katika shule hizo.

Mimi na wewe hatufahamu nini tatizo la matokeo hayo, yawezekana walimu wanatimiza wajibu wao kikamilifu kwa kuwafundisha wanafunzi vizuri au pia yawezekana hawakutimiza wajibu wao, ni jukumu lao sasa kujitizama wakijiuliza wanategemea kizazi hicho ni nini hatma yake.

Pia yawezekana wanafunzi ndiyo changamoto kutokana na mazingira ya sasa ya mjini ambapo watoto wengi wamekuwa wakijifunza mambo mengi ya mtaani na kukariri ‘miziki’ badala ya masomo, lakini pia suala la kumomonyoka kwa maadili likiwa ni tatizo kuu.

Tukifuatilia kwa umakini, jambo hilo na kuzungumza na walimu na wanafunzi tunaweza kwa pamoja kutambua changamoto zilizozikabili shule hizo na jinsi ya kukabiliana nazo au jinsi ya kuzitatua ili kuboresha elimu kwa kizazi kijacho.

Naamini jitihada za makusudi zikifanyika matokeo yajayo shule hizo zinaweza kufanya mapinduzi makubwa na wanafunzi wake kupata alama na wastani wa kuridhisha. Hii pia itasaidia kukuza kiwango cha elimu nchini pamoja na kuongeza ushindani katika elimu.