Washiriki netiboli Afrika Mashariki jipange vizuri

MASHINDANO ya netiboli ya Afrika Mashariki yatafanyika jijini Nairobi nchini Kenya kuanzia Aprili 23 hadi 30 mwaka huu.

Tanzania katika mashindano hayo inatarajia kuwakilishwa na timu tatu za Uhamiaji, JKT Mbweni na Jeshi Stars huku timu za Zanzibar zikiwa ni JKU, Mafunzo na Zima Moto. Mashindano haya ni makubwa kwa mchezo huu katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikishiriki, lakini haina mafanikio.

Mafanikio yenyewe tunayoyazungumzia hapa ni kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, ambayo pamoja na kushiriki mara nyingi, lakini imeshindwa kulitwaa taji hilo kwa muda mrefu. Tunakumbuka huko nyuma wakati Jeshi Stars ilipokuwa Jeshi Stars au JKT Mbweni ni JKT Mbweni kweli sio sasa, ambapo timu hizo zote hazina ubavu tena wa kutamba kimataifa.

Na sio kimataifa tu hata hapa nchini kwa miaka kadhaa zimeshindwa kufurukuta na badala yake Uhamiaji ndio imeshika chati kwa kuchukua ubingwa wa taifa na ilikuwa mshindi watatu katika mashindano yaliyopita ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika Uganda.

Pamoja na timu hizo kutofanya vizuri kwa miaka kadhaa sasa, lakini katika michezo hakuna lisilowezekana ila tu kinachotakiwa ni kujipanga na kufanya mazoezi vizuri ili kufanya vizuri. Miezi miwili iliyobaki kabla ya kuanza kwa mashindano hayo ya netiboli sio mbali, hivyo wawakilishi wetu wanatakiwa kujifua vilivyo ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano hayo.

Kwa kweli tumechoka kuwa wasindikizaji kila mwaka na sasa wakati umefika wa kufanya vizuri katika mashindano ya mwaka huu na kurejea na ubingwa. Tanzania imekuwa ikifanya vibaya katika mashindano mbalimbali ya kimataifa iwe netiboli, mpira wa kikapu, judo, riadha na michezo mingine na sababu kubwa ni kutojiandaa vizuri na kwa wakati.

Uhamiaji, JKT Mbweni pamoja na Jeshi Stars tumieni vizuri muda huu uliobaki kwa kufanya mazoezi kwa bidii na kurekebisha makosa madogo madogo yaliyopo katika timu zenu ili muweze kufanya vizuri. Tumechoka kila mwaka kuwa wasindikizaji hata katika netiboli, kwani huko nyuma timu zetu za Bima, Bandari na hata hao Jeshi Stars na JKT Mbweni zilikuwa zikifanya vizuri hata kimataifa.

Ni matarajio yangu kuwa wawakilishi wetu wa kimataifa katika mashindano hayo ya Afrika Mashariki watafanya vizuri mwaka huu na kututoa kimasomaso kwa kurudi nchini na Kombe. Kamwe hakutakubali kusikia visingizio vya kila mwaka kuwa waamuzi waliziuma timu zetu au zilichelewa kuanza mazoezi mapema, kwani tayari ratiba mmeshapata ya kuanza kwa mashindano hayo.

Huu ni wakati wa kuangalia tulijikwaa na sio pale tulipodondokea kwani tukifanya hivyo basi bila shaka tutaweza kurekebisha makosa yetu vizuri na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Kazi kwenu Uhamiaji, JKT Mbweni, Uhamiaji pamoja na wenzenu wa Zenji, Mafunzo, JKU na Zima Moto hatutaki visingizio.