20Mei2013

 

Watanzania wanasubiri bajeti nafuu

BAJETI ya Serikali ya mwaka wa Fedha 2012/13 inatarajiwa kusomwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa Alhamisi, huku masikio ya kila Mtanzania yakielekea Dodoma kusikia ambacho Serikali inakusudia kutumia katika maendeleo ya nchi.

 

Baada ya kusomwa Bajeti hiyo, fursa itatolewa kwa wabunge kuijadili kwa kina kabla ya kuipitisha, lengo likiwa ni kuirekebisha na kuiweka sawa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Wadau mbalimbali wamekuwa wakiichambua bajeti hiyo na kuiona kama imelenga kukomboa wananchi na hasa wale wa chini na kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Ni imani yangu kuwa bajeti ya mwaka huu itakayosomwa kukiwa na uongozi mpya itakuwa tofauti na miaka ya nyuma, kwa kuhakikisha inazingatia vipaumbele vya Serikali katika kuinua uchumi na itazingatia kupanda kwa hali ya maisha ya wananchi wa hali ya chini na hasa wa vijijini na kutokuwa ya kisiasa.

Tunaposema bajeti isiwe ya kisiasa ni kumaanisha tunataka bajeti itakayoangalia jinsi ya kutatua matatizo ya wananchi yanayotokana na upandaji wa maisha na isiyo ya kuorodhesha mambo yasiyotekelezeka na ambayo hayana msaada kwa wananchi.

Mambo ambayo tunatakiwa kuyaona yakipewa kipaumbele ni yanayogusa sekta ya kilimo ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi unaoweza pia kuinua wananchi wa hali ya chini.

Pia tunataka kuona bajeti ambayo kwa kiasi kikubwa isiyotawaliwa na wahisani na badala yake ibainishe mbinu za kupata fedha kutoka vyanzo vya ndani kama vile kuwa na mfumo mzuri wa ukusanyaji kodi, kwani mapato mengi yanapotea kwa kukosa mfumo.

Pia rasilimali nyingi kama madini zimekuwa hazitoi mchango mkubwa kama inavyotakiwa na hili ni kutokana na mikataba ambayo hainufaishi Taifa.

Ni matumaini ya wengi kuona bajeti ijayo inafuta misamaha ya kodi ambayo haina tija, mfano mzuri Serikali kwa nia njema ilitoa msamaha wa kodi wa kampuni ambazo zitaingiza sukari kutoka nje lengo likiwa ni kumsaidia mwananchi kuhakikisha bei ya sukari inapungua kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo suala hilo limekuwa kichekesho, bei haijapungua huku Serikali ikiwa imepoteza mapato ambayo yangesaidia nyanja nyingine.

Pia kuangalia upya kodi za mishahara ya wafanyakazi kutoka asilimia 14 ili ishuke zaidi ingawa kwa muda mrefu, Serikali inaona kuwa ndicho chanzo kimojawapo cha mapato, jambo ambalo linafanya nyanja nyingine kuachwa bila kuchangia kitu chochote.

Si hivyo tu, pia ni matarajio ya Watanzania kuona bajeti ambayo inalenga kuondoa tatizo la umeme ambalo limekuwa kero nchini, upatikanaji wa maji safi kwa wananchi, sekta ya afya kwa kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya, ambavyo ni mkombozi wa mwananchi wa kawaida mijini na vijijini.

Pia inatakiwa bajeti itakayolenga kupunguza bei ya mafuta ya petroli, dezeli na ya taa na kupunguza matumizi ya Serikali na kuifanya kuwa bajeti ya wananchi.

y>