Mgogoro wa walimu utatuliwe kabla ya madhara
- Imeandikwa tarehe 13 Juni 2012
- By Lucy Lyatuu
- Imesomwa mara: 886
MWANZONI mwa mwezi huu, Baraza la Taifa la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) lilitangaza mgogoro wa kikazi wa walimu na Serikali likitaka walimu walipwe madai yao ndani ya mwezi mmoja, la sivyo uitishwe mgomo wa nchi nzima mara moja.
Suala la kutaka kuitisha mgomo si mara ya kwanza linasikika kutoka kwa walimu hao wakidai mishahara, jambo ambalo limekuwa likiwakwaza kwa kipindi kirefu bila ya kupatiwa ufumbuzi stahiki.
Walimu wanaitaka Serikali iwaongeze mishahara ya mwezi kwa asilimia 100, kulipa posho ya kufundishia kwa mwezi kwa walimu wa masomo ya Sayansi kwa asilimia 55 na wa masomo ya Sanaa asilimia 50.
Vile vile Baraza linaitaka Serikali ilipe posho ya mazingira magumu kwa walimu wanaofanya kazi kwenye wilaya zenye mazingira magumu kwa mwezi kwa kiwango cha asilimia 30.
Rais wa CWT, Gratian Mkoba anasema mgogoro huo umetangazwa kwa mujibu wa kifungu cha 80 (1) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 na utakuwa wa kimaslahi na kwamba endapo maafikiano hayatafikiwa, mgomo utaitishwa ili kushinikiza Serikali itekeleze matakwa ya walimu kama inavyoelekeza sheria.
Kwa sasa inafahamika kuwa shule nyingi pamoja na vyuo vimefungwa kwa mapumziko ya katikati ya mwaka, ambapo walimu wameamua kutumia muda huo kusimamia kilio chao kiweze kusikilizwa na muafaka upatikane.
Wanafanya hivyo ili waanzapo muhula mwingine wa masomo, wawe katika hali nzuri ya ufundishaji, huku wakikumbuka kuwa wazazi nao wanahangaika kutafuta ada na vifaa vingine vya shule kwa watoto wao, wakiamini watarudi shuleni kuendelea vema na masomo.
Hakuna atakayebisha kuwa kama hali ya kifedha haitakuwa nzuri miongoni mwa watumishi ni wazi utendaji hautakuwa wenye weledi na kuna uwezekano wa kazi kuharibiwa au kutofanyika kwa kiwango stahiki, ambapo inaweza kuwa na faida na matunda kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, ni vyema kwa mgomo huo kuepushwa na suluhu kufikiwa, kwani Watanzania hawajasahau vidonda vilivyotokana na mgomo wa madaktari wa nchi nzima na ambao uliathiri wagonjwa wengi ambao hawakuwa na uwezo wa kupata matibabu katika hospitali binafsi ambazo matibabu yake yanahitaji fedha nyingi.
Katika mgomo huo wa madaktari ambao ulikuwa na madai yao, majadiliano yalifanyika baada ya wagonjwa kuhangaika wakitafuta huduma ya afya kwa haraka katika sehemu mbalimbali na wengine kujikuta wakizidiwa majumbani mwao.
Ni imani yangu, kuwa ngazi zinazohusika zitafuatilia madai ya walimu ili kuepusha mgomo ambao endapo ukitokea waathirika wakubwa watakuwa ni watoto wa Watanzania wengi ambao hawasomi katika shule za binafsi.
Aidha, kutofikiwa haraka kwa makubaliano baina ya pande hizo, kunaweza kuwa chanzo cha ongezeko la idadi ya watoto wanaofeli mitihani yao huku Serikali ikijitahidi kupambana na umasikini kwa kuongeza shule nyingi zitakazohakikisha ufaulu unaongezeka mwaka hadi mwaka.
Kwa upande mwingine, kutotekelezwa kwa madai hayo ya walimu kunaweza kuwavunja moyo na kuwanyima hamasa ya kufundisha wanafunzi kwa moyo na kujikuta jamii ikilalamika kila mara kuona wanafunzi wakifeli bila kujua tatizo linalochangia.


