Sakata la sensa lishughulikiwe kwa busara
- Imeandikwa tarehe 14 Juni 2012
- By Halima Mlacha
- Imesomwa mara: 1026
KWA takribani wiki mbili sasa, habari zinazotawala vyombo vya habari ni suala la Waislamu nchini kususia kushiriki Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika nchini Agosti.
Sababu kubwa ya taasisi hiyo ya dini kuchukua uamuzi huo ni kutokana na uamuzi wa Serikali kukataa kuingiza kwenye dodoso za sensa kipengele cha dini, hali ambayo Waislamu wanaamini itawezesha kupatikana kwa takwimu halisi ya Watanzania kidini.
Msimamo huo ulianza kutolewa mapema mwezi huu kama onyo kwa Serikali na mashekhe nchini wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu, Shehe Ponda Issa Ponda ambapo jana kupitia Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu nchini, Shekhe Mussa Kundecha walitangaza rasmi mgomo wa kutoshiriki sensa.
Onyo la awali mashekhe hao ambao pia wameungwa mkono na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), liliitaka Serikali iingize kipengele hicho kutokana na kwamba hadi sasa Tanzania haina takwimu halisi za Watanzania kidini.
Na mfano halisi uliotolewa na Shehe Ponda akinukuu vyombo vilivyotoa takwimu hizo ni tovuti ya Wakatoliki inayoonesha kuwa mwaka 2008 Waislamu walikuwa asilimia 34, Wakristo asilimia 44 na Wapagani asilimia 22.
Aidha, akaitaja Televisheni ya Taifa (TBC) ambayo hivi karibuni iliripoti kuwa Waislamu ni asilimia 32, Wakristo asilimia 52 na Wapagani asilimia 16 wakati Idara ya Uhamiaji ikionesha kuwa mwaka 2010 Waislamu walikuwa asilimia 35, Wakristo asilimia 32 na Wapagani asilimia 33.
Pamoja na hayo, alisema pia chapisho la Serikali la Ramani ya Taifa linaonesha kuwa mwaka 2011 Waislamu walikuwa asilimia 35, Wakristo asilimia 45 na Wapagani asilimia 20.
Kwa hoja za mashekhe hao, kuingizwa kwa kipengele hicho kutamaliza mzozo na kudhibiti taasisi zisizo rasmi katika takwimu, kutoa takwimu zisizo sahihi lakini pia itasaidia taasisi za dini nchini kusaidia waumini katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kidini.
Hata hivyo, ombi hilo lilikataliwa rasmi awali na Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na jeneza lake kupigiliwa msumari na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira.
Kwa msimamo huo wa Serikali, Waislamu wamekuja juu na kutangaza rasmi kutoshiriki sensa zikiwa zimebaki takribani zaidi ya siku 30 ianze kutekelezwa, hadi pale ombi lao litakapofanyiwa kazi.
Cha msingi hapa, ni kwa pande zote mbili kuwa makini na kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa busara bila jazba au shinikizo, ili kufikia msimamo utakaokuwa na manufaa kwa Watanzania bila kuathiri imani zao na amani iliyopo.
Sensa ina umuhimu kwa nchi husika kwa kuwa ndiyo inayotoa dira kwa Serikali kuwa ina idadi gani ya watu, kitakwimu, kimaendeleo na hapo ndipo hata mipango ya uchumi huanza kupangwa ili kuweza kumwinua mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa jumla.
Hakuna asiyejua, kuwa suala la dini ni nyeti na utekelezaji wake hauhitaji kukurupuka, Watanzania kwa sasa macho yao yapo kwa pande hizo mbili yakitaka kuona ufumbuzi wa suala hilo unapatikana na hivyo ni matarajio ya wengi kuwa Waislamu watalegeza msimamo wao na kuipisha Serikali kulifanyia kazi vema ombi lao.
Lakini pia wakati huo huo, ni matumaini ya Watanzania kuwa Serikali nayo itakuja na ufumbuzi mwafaka kuhusu ombi hilo, bila kusababisha mvurugano au malumbano ambayo yanaweza kusababisha nchi ikashindwa kutekeleza suala hilo muhimu la Sensa ya Watu na Makazi.


