WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa taarifa ya awali kuhusu majeruhi Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, ambapo amesema hadi sasa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke imepokea majeruhi 30 na kwamba mwanaume mmoja mwenye umri wa takribani miaka 40 amefariki.
Ummy amesema: “Majeruhi wengi wanaendelea vizuri wana majereha madogomadogo, wanaendelea na vipimo, aidha timu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ipo uwanjani, inafuatilia kwa karibu kuangalia kama kuna majeruhi wengine”
Japokuwa Wizara ya Afya bado haijasema mtu huyo alifariki katika mazingira yapi, baadhi ya mashabiki leo kabla ya mechi kuanza walionekana wakiruka uzio na wengine kuvunja geti na kuingia uwanjani hapo, huku wengine wakiingia kwa kusukumana kupitia moja ya mageti ya uwanja huo kutaka kushuhudia mchezo wa fainali ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga na USM Alger ya Algeria iliyomalizika kwa wenyeji kulala mabao 2-1.