10,000 kunufaika na ukarabati wa tangi la maji

WANANCHI zaidi ya 10,000 wanaoishi katika mitaa ya Mgaza na Kasanga, Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro sasa watapata maji ya kutosha baada ya kukamilika kwa ukarabati mkubwa wa tangi la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 135,000 katika eneo la Kasanga.

Serikali kupitia Wizara ya Maji ilitoa fedha zaidi ya Sh milioni 600 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa tangi na uwekaji wa mabomba yenye kipenyo kikubwa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Morogoro, (MORUWASA), Tamimu Katakweba jana baada ya kukagua bomba la maji kwa umbali wa zaidi ya kilometa sita kutoka kituo cha kusafisha na kutibu maji cha Mafiga hadi lilipojengwa tangi hilo mlima wa Kasanga.

Advertisement

Mhandisi Katakweba alisema kuwa kukamilika kwa mradi wa ukarabati huo utawaondolea wananchi hao mgao wa maji wa mara moja baada ya siku kumi hadi 14 na kupata maji kila baada ya siku moja.

Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata hiyo akiwemo Katibu Mwenezi wa kata, Christina Adamu, waliofika kwenye tangi hilo na kushuhudia maji yakiingia wameishauri mamlaka hiyo kuwapa taarifa viongozi ya kile kinachoendelea ili nao kutoa mrejesho kwa wananchi na kupunguza malalamiko.

“Shida kubwa ya wananchi ni maji, yakipatikana hakuna ugomvi, mwanzo tulisikia hayafiki kwenye tangi, lakini nimejiridhisha yanafika, kuona ni jambo jema,” alisema Christina.

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *