Bashungwa atamani makubwa zaidi michezoni

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Innocent Bashungwa amesema wizara  yake itaendelea kushirikiana Wizara ya  Utamaduni, Sanaa na Michezo kufikia dhamira ya serikali  kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Kombe la Dunia.

Bashugwa amesema hayo Desemba 19, 2022,  wakati akipokea vikombe vya ushindi vilivyotwaliwa timu ya michezo ya Shirika la Mzinga linalomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ), katika michuano mbalimbali kwa msimu wa mwaka  2022, ikiwemo Shimiwi na kuibuka washindi wa jumla.

“Dhamira  ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, ikiwemo Kombe la Dunia kama alivyobainisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo  Mohammed Mchengerwa, kwa hiyo kama mnavyojua kwenye timu zetu za majeshi kuna vipaji vingi sana, vinaendelea kunolewa, hivyo tutashirikiana kupitia Baraza la Michezo kuona namna tunafanikiwa kufikia  malengo,”  alisema Bashungwa.

Waziri Bashungwa aliwapongeza wachezaji wa shirika hilo kwa hatua waliyoifikia na kuipatia sifa  wizara na jeshi kwa ujumla.

“Timu za majeshi  likiwemo JWTZ zimekuwa zikifanya vizuri hata kwenye michuano ya kimataifa na kuiwakilisha nchi vyema,”alisema Waziri Bashungwa.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Faraji Mnyepe  alizitaka timu za michezo zilizopo chini ya wizara hiyo kuwekeza zaidi katika kufanya mazoezi na maandalizi ya kutosha ili zifanye vizuri na kuachana na dhana ya kutegemea kamati za ufundi (ushirikina).

Alisema dhana ya kutegeme kamati ya ufundi haijawahi kuisaidia timu yeyote au mchezaji yeyote kufikia mafanikio, bali ni juhudi na mazoezi na maandalizi ya uhakika  kama ilivyofanya timu ya Shirika la Mzinga.

“Nawapongeza  kwa kufanikiwa kushinda vikombe hivi,  lakini bado sijaridhishwa na ushindi wa pili na watatu, kwa hiyo nawapa changamoto katika mashindano yajayo kushinda nafasi ya kwanza katika kila mchezo, hivyo mnatakiwa kujiandaa vyema kwa sababu ushindi unaanza kuonekana katika uwanja wa mazoezi na sio kama  ya kamati ya ufundi,” alisema Dk Mnyepe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Michezo wa shirika la Mzinga, David Msami alisema, ushindi wa jumla umepatikana baada ya kushinda vikombe 10 katika michezo mbalimbali waliyoshiriki.

Habari Zifananazo

Back to top button