13 wakamatwa wakituhumiwa kuchakachua mbolea

JESHI la Polisi mkoani Njombe limekamata watu 13 wanaotuhumiwa kuhusika kuchakachua mbolea za ruzuku na kuwauzia wakulima.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa watu hao walikamatwa baada ya msako wa takribani wiki mbili.
“Katika sakata hili, wamekamatwa watuhumiwa 13, akina mama wawili, vijana pamoja na mfanyabiashara ambaye awali alitoroka lakini hivi sasa ametiwa mbaroni na yupo polisi na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hili,” alisema Kamanda Issah.
Kamanda Issah alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya taarifa za awali kutolewa kwa jeshi hilo juu ya mbolea feki kuuzwa kwa wakulima.
“Mnamo Januari 12, mwaka huu, kulitolewa taarifa kuwa kuna mbolea isiyo sahihi inauzwa katika mitaa ya Mgodechi na Kwivaha, tulienda Jeshi la Polisi na viongozi, tukakuta mifuko hiyo, ufuatiliaji ulifanyika na tukagundua store (ghala) ya kuchakachua mbolea ambapo tulikuta mifuko nusu nusu ya mbolea 70 na mitupu inayozidi 10,000, na mifuko mingine mipya, mabalo manne yanayoonekana kutoka kiwandani,” alisema.