Kuhusu HabariLEO

Kuhusu HabariLEO

HabariLEO ni gazeti la kila siku la Kiswahili ambalo limejikita katika kuchapisha Habari za kweli, na ukweli mtupu kwa kuzingatia misingi na viwango vya juu vya taaluma ili kupasha habari, kuburudisha na kuelimisha wasomaji mijini na vijijini.

Gazeti la HabariLEO limekuwa likichapishwa tangu toleo lake la kwanza la Desemba 21, 2006 likiwa ni sehemu ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali, “Tanzania Standard (Newspapers) Limited (TSN).” HabariLeo ni gazeti pekee la habari la serikali linalochapisha taarifa na habari zake kwa kiswahili na ambalo limekuwa sokoni kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Uamuzi wa kuanzisha gazeti la HabariLEO ulitokana na utashi wa kisiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM). CCM kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2005 hadi 2010 iliweka lengo, pamoja na mambo mengine kuanzisha gazeti la Kiswahili la Serikali. Kifungu cha 116 (C) cha Ilani ya Chama Tawala kinasema “Kwa kuzingatia mchango mkubwa unaotolewa na vyombo vya habari katika jamii, katika kipindi cha 2005–2010 CCM itazitaka Serikali … Kuanzisha gazeti la Kiswahili la Serikali.”

Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete alisema Gazeti la HabariLEO linapaswa kuhakikisha habari zake ni za kweli, ukweli mtupu hata kama unauma. Uzinduzi wa gazeti hili ulifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM mjini Dodoma, asubuhi ya Desemba 21, 2006.

Mwaka 2009, Gazeti la HabariLEO lilikuwa moja ya Magazeti nchini Tanzania yaliyoanzisha tovuti. Tovuti ya kwanza ilikuwa ikifahamika kama www.habarileo-tsn.co.tz na ilibadilishwa nakuwa www.habarileo.co.tz ambayo inatumika hadi sasa. Tovuti hii ilianzishwa, pamoja na mambo mengi kuhakikisha watanzania na watumiaji wengine wa lugha ya kiswahili wanapata habari, taarifa na mawazo mbalimbali kuhusu Tanzania na Ulimwengu kwa lugha adhimu ya Kiswahili. Tovuti hii imefanyiwa maboresho makubwa mwezi Julai 2022 na Novemba 03, 2024 ili kuakisi mahitaji ya sasa na ya badae ya ulimwengu wa kidigitali. HabariLEO imeendelea kujiimarisha ikijengwa na misingi mikuu ambayo ndiyo Tunu za Kampuni; Kasi, Teknolojia, Ubunifu, Mwitikio na Uwajibikaji.

Kuhusu Umiliki

HabariLEO linamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kampuni ya Magazeti ya Serikali–TSN. Kwa mujibu wa Muundo mpya, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu ambaye anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile kuna Bodi ya Wakurugenzi ambayo Mwenyekiti wake huteuliwa na Rais wakati wajumbe wa Bodi hiyo huteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya Habari.

Kuhusu Uongozi

Katibu Mkuu wa Zamani katika Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. Hab Mkwizu ndiye Mwenyekiti wa Bodi. Tuma Abdallah ni Mkurugenzi Mtendaji na unaweza pata taarifa zaidi kuhusu uongozi wa kampuni ya Magazeti ya Serikali hapa http://www.tsn.go.tz Mhariri wa Kwanza wa Gazeti hili ni Cassian Malima, Mhariri wa Habari wa kwanza alikuwa Titus Kaguo, ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi TSN na Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Uhariri (Editorial Committee). Mhariri wa Makala wa kwanza alikuwa Nicodemus Ikonko, Mgaya Kingoba, ambaye kwa sasa ni Kaimu Meneja wa Huduma za Habari za Kiswahili TSN alikuwa Mhariri wa Kwanza wa Michezo.

Uwazi HabariLEO

HabariLEO hupokea kiasi cha msaada wa kifedha kutoka Serikali Kuu na kwa sasa inawaomba Watanzania, Taasisi na Umma kwa ujumla kusaidia uandishi bora wa habari kupitia uanachama maalum. Vyanzo vingine vya mapato ni mahusiano ya kibiashara hasa matangazo na mauzo ya nakala na gazeti mtandaoni (TSN e-Paper).