15 kufanyiwa upasuaji wa kisasa MOI

15 kufanyiwa upasuaji wa kisasa MOI

WAGONJWA 15  wa magonjwa  ya ubongo na uti wa mgongo watafanyiwa upasuaji kwa siku tano katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI)  ikiwa ni hatua ya kuwajengea uwezo wa kisasa zaidi wataalamu wa ndani.

Akizugumza wakati wa mafunzo hayo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respisius Boniface, alisema mafunzo hayo ya kimataifa ya siku tano yameandaliwa na MOI na Chuo Kikuu cha Well conel cha Marekani.

Dk Boniface amesema yatahusisha mafunzo ya nadharia na vitendo, ambapo wanategemea wagonjwa tisa mpaka 15 watafanyiwa upasuaji.

Advertisement

“Kikubwa tunachotegemea  ni matumizi ya mashine, ambazo wamekuja nazo ambazo kama taasisi hatuna, wamekuwa wakija nayo na kuondoka nayo, lakini sasa itabaki kwetu,” amesema.

Amebainisha kuwa mashine hizo kazi yake kubwa kuongeza umakini, wakati wa upasuaji na inapunguza muda wa upasuaji  na inatumika kwenye uti wa mgongo.

“Tunafanya saa tatu hadi nne, lakini kwa mashine hii ni saa moja au moja na nusu, mashine nyingine inatumika kwa upasuaji wa mgongo na ubongo kama kunyoosha vibiongo mashine hizo zitahakikisha upasuaji unafanyika kwa usalama ,”amesisitiza.

Amesema kupitia wataalamu waliofika katika mafunzo hayo kutoka Marekani, watafanya upasuaji wa kisasa ambao unafanyika katika nchi zingine zilizoendelea.

 

Amesema kumekuewa na ongezeko la wagonjwa kwa asilimia tano hadi sita kwa mwaka, lakini kubwa zaidi ni ajali wengi wanaoenda  hasa  ni wa ajali za pikipiki kwa sababu wengi hawapendi kuvaa kofia ngumu.

“Sababu nyingine ya kuongezeka kwa wagonjwa ni mashine za utambuzi, sasa serikali inatawanaya CT scan ipo maeneo mengi na wagonjwa wanaongezeka baada ya kugunduliwa wanaletwa,” amesema.

Amefafanua kuwa wagonjwa wa ajali wanaongezeka kwa asilimia tano mpaka 10 na uvimbe asilimia mbili hadi tatu.

Dk Boniface amesema kwa siku wanapata wagonjwa wa ajali kati ya 10 hadi 15 na kwa  mwezi 350 hadi 400, huku asilimia 70 ni ajali za bodaboda na waliobaki ni ajali zingine.