ZAIDI ya wakazi 16,104 wa vijiji vitano Kata ya Karabagaine Wilaya ya Bukoba, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama.
Hatua hiyo inatokana na kukamilika awamu ya kwanza ya mradi wa maji wa Karabagaine unakotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa Mazingira (BUWASA) uliogharimu zaidi ya Sh Milioni 550.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Meneja wa BUWASA, Julieth Shangali katika maadhimisho ya wiki ya maji, alisema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa awamu mbili na kwamba utakapokamilika utakuwa umegharimu kiasi cha Sh bilioni 1.8 na wanachi watakaonufaika baada ya mradi kukamilika watakuwa 25,877.
“Mradi wa maji wa Karabagaine umezingatia vigezo vyote na maji haya ni salama kwa matumizi yote ya nyumbani, tayari awamu ya kwanza imekamilika, “alisema Shangai.
Kwa upande Kaimu Meneja wa RUWASA mkoani Kagera, Mhandisi Patrice Jerome, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, jumla ya miradi 31 yenye thamani ya Sh Bilioni 13 imetekelezwa katika Vijiji 45 na kuwanufaisha wananchi 152,541, huku vituo vya kuchotea maji 382 vikiwa vimejengwa.
Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila, alipongeza juhudi zinazofanywa na mamlaka zilizopewa jukumu la kuisimamia miradi ya maji mkoani Kagera na kuwapatia wananchi huduma bora.
Alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha miradi inayokabidhiwa kwao inalindwa na kutunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo, ikiwemo wananchi kuchangia malipo ya bili, kutofanya shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji.