Mfumo mpya kupima utendaji wa watumishi utaongeza uwajibikaji

KUANZISHWA kwa mfumo mpya wa kupima utendaji kazi kubaini mikoa na halmashauri zinazoongoza kukwepa kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi, kutaongeza uwajibikaji.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama mfumo mpya wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma utatumika kubaini mikoa na halmashauri ambazo zinaongoza kwa kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi.

Jenista anasema mfumo huu mpya utawalazimisha watumishi hao kuwasilisha barua kwa Katibu Mkuu Utumishi kuomba ufafanuzi wa masuala ambayo mikoa na halmashauri hizo zina uwezo wa kutoa ufafanuzi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo.

Ufafanuzi huu wa mfumo, aliutoa wakati akizungumza na wanasheria na maofisa utumishi kutoka katika Sekretarieti za mikoa na halmashauri za wilaya juzi.

Hii ilikuwa ni kabla ya kufungua kikao kazi cha maofisa hao kilicholenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

Jenista akasema mfumo huo utawaweka kwenye kundi la kutowajibika watumishi wote watakaosababisha mikoa na halmashauri zao kukwepa jukumu la kutoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa kusingizia kuwa masuala hayo yanapaswa kutolewa ufafanuzi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Tunaamini kuwepo kwa mfumo huu mpya sasa utawawezesha watumishi kuwajibika ipasavyo kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan imeshajipambanua katika uwajibikaji kwa kila Mtanzania, awe mtumishi wa umma au wa sekta binafsi.

Jenista anahoji ni kwa nini mwajiri amwandikie barua Katibu Mkuu-Utumishi kuomba ufafanuzi wa jambo wakati mwajiri huyo anaye Ofisa Utumishi ambaye akishirikiana vizuri na Mwanasheria, kwa kutumia nyaraka zilizopo wana uwezo mkubwa wa kulitolea uamuzi jambo ambalo linaombwa kutolewa ufafanuzi na Katibu Mkuu-Utumishi?

Ni ukweli ulio wazi kwamba maofisa utumishi na wanasheria mnapaswa kushirikiana katika kutoa ufafanuzi na kufanya maamuzi ya masuala ya kiutumishi kwa mujibu wa kanuni, sheria, taratibu na miongozo ya kiutumishi iliyopo badala ya kukwepa jukumu hilo.

Kiongozi yeyote wa utumishi anawajibika katika nafasi aliyopewa ili kumwakilisha aliyemteua katika nafasi aliyopewa. Kukwepa majukumu yake na kuyasukuma mbele kumekuwa kukikwamisha jitihada za serikali za kuona kila mtumishi anawajibika katika nafasi aliyopewa. Mfumo huu mpya sasa utakuwa mwarobaini kwa watumishi ambao wameaminiwa kushika nafasi kubwa lakini wamekuwa hawapendi kuwajibika kwa nafasi zao badala yake, wanasubiri ofisi ya Katibu Mkuu-Utumishi itoe ufafanuzi badala yao.

Tunaamini Ofisi ya Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma itakuwa inatoa ufafanuzi katika masuala makubwa ambayo ofisi za wilaya na halmashauri kiuhakika haziwezi kutolea ufafanuzi.

Kwa kuwa maofisa utumishi na wanasheria kutoka sekretarieti za mikoa 16 na halmashauri za wilaya 84 wote wamepikwa katika hili, tunategemea matokeo chanya nchi nzima kwa kuongeza uwajibikaji zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button