Zanzibar wajipanga kutumia vyema fedha za ‘Heshimu bahari’

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imejipanga vizuri kutumia fedha za mradi wa ‘Heshimu bahari’ unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la misaada la Kimataifa la Marekani (USAID) ambao umelenga kuimarisha mazingira ya baharini na viumbe vyake katika maeneo ya hifadhi.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu, Aboud Suleiman Jumbe wakati alipozungumza na HabariLEO kutokana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata fedha jumla ya dola za Marekani milioni 8.4 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao utahusisha Zanzibar pamoja na Tanzania Bara.

Alisema mradi huo wa miaka mitano ulitambulishwa rasmi katika ziara ya Makamu wa kwanza wa Rais wa Marekani, Kamala Harris. Jumbe alisema mradi huo utasimamiwa na Taasisi ya Chemonic, lengo lake kubwa ni kukuza hifadhi ya bahari na kuongeza uzalishaji zaidi katika rasilimali za baharini na mazalia ya samaki.

Alisema mradi huo utahusisha jumla ya maeneo manne ikiwemo kuunga mkono usimamizi shirikishi wa maeneo ya hifadhi ya bahari kwa kushirikiana na serikali pamoja na jamii. Aidha, alisema mradi huo utafanya kuimarisha maeneo ya hifadhi ya ikolojia pamoja na maeneo ya hifadhi ikiwemo Minca, Minai, Tumka pamoja na PECCA iliyopo Pemba.

Alifahamisha katika mradi wa ‘Heshimu bahari’ utasaidia juhudi za serikali katika kuanzisha hifadhi mpya ya bahari katika upande wa Mashariki ya Kisiwa cha Pemba wenye utajiri mkubwa wa rasilimali.

 

‘’Mradi huu umelenga kuona kwamba maeneo ya hifadhi ya bahari yanaimarishwa na kulindwa, lakini pia umelenga kuanzisha maeneo mapya zaidi,’’ alisema.

Aidha, alifahamisha mradi huo utasaidia kushajihisha uwekezaji zaidi wa hifadhi za bahari kupitia sekta binafsi, hatua ambayo itaongeza mapato ya serikali.

Dk Jumbe alizitaja faida za mradi huo ni pamoja na kuwainua vijana ikiwemo akinamama katika kulima mazao ya baharini ikiwemo mwani na kuliongezea thamani pamoja na masuala ya utafiti kwa ujumla wake.

Mradi wa Heshimu bahari unatarajiwa kutekelezwa kwa upande wa Zanzibar ambapo kwa Tanzania utafanya kazi katika wilaya za Bagamoyo, Mkinga, Pangani na Dar es Salaam.

Mradi huo unatarajiwa kutumia dola za Marekani milioni 8.4 katika awamu ya kwanza ambapo fedha hizo zitaongezwa hatua kwa hatua hadi kufikia dola za Marekani milioni 12.9.

Jumbe alisema Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu ipo katika hatua za mwisho za kupitia sheria ya uvuvi ya mwaka 2010 kwa ajili ya marekebisho ambapo mchakato huo tayari umepitia katika ngazi mbalimbali ikiwemo wadau kutoa maoni ya sheria hiyo ikiwemo wavuvi.

Habari Zifananazo

Back to top button