SERIKALI imesema shughuli za uvuvi zinafanywa zaidi na wavuvi wadogo kwenye maji ya asili, ambapo huchangia takriban asilimia 95 ya samaki wote wanaovuliwa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
“Hadi Aprili, 2023, jumla ya wavuvi wapatao 197,763 walishiriki moja kwa moja katika shughuli za uvuvi kwa kutumia vyombo vya uvuvi vipatavyo 58,448 na kuwezesha kuvuna tani 426,555.46 za samaki zenye thamani ya Shilingi trilioni 2.86.
“Kati ya hizo, tani 381,113.22, sawa na asilimia 89 ni kutoka maji baridi na tani 45,442.24, sawa na asilimia 10.7 ni kutoka maji chumvi,” amesema Waziri Ulega.
Amesema katika mwaka 2022/2023, serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi, ili kuvutia uwekezaji katika uvuvi wa kibiashara ambao hufanyika katika maji ya kitaifa kwa kuhusisha uvuvi wa kambamiti na ukanda wa uchumi wa bahari.
“Mazingira hayo yamewezesha Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari kuu kutoa leseni kwa meli 48 kwa ajili ya kuvua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari (EEZ). Kati ya hizo, meli 45 ni za kigeni na meli tatu ni za ndani.
“Aidha, uvuvi wa kambamiti hufanyika kwa msimu kuanzia mwezi Machi hadi Septemba, katika kanda ya Kaskazini maeneo ya Bagamoyo, Saadani na Pangani na mwezi Aprili hadi Agosti katika Kanda 70 ya Kusini maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Kilwa kila mwaka.
“Katika msimu wa mwaka 2023, jumla ya meli tisa ziliomba vibali vya kuvua kambamiti kati ya hizo, meli nne zimekidhi vigezo na kupewa leseni. Katika msimu wa uvuvi – mwaka, 2022 jumla ya meli sita zilizopewa leseni zilivua tani 57.59 za kambamiti zenye thamani ya shilingi milioni 835.04,” amesema Waziri Ulega.