21 mbaroni tuhuma wizi wa kimtandao

MANYARA: Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara linawashikilia watu 21 kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu wa makosa ya kimtandao ikiwemo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kinyume cha sheria.

Hayo ameyasema Kamanda wa Polisi mkoani Manyara Kamishna Msaidizi wa (ACP), George Katabazi Januari 11, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusema watuhumiwa hao wamekamatwa katika kipindi cha mwezi Desemba 2023 mpaka sasa.

Aidha, amesema watuhumiwa hao wamekutwa na vielelezo mbalimbali ikiwemo mavazi ya wakala wa watoa huduma za simu, line za simu zilizobatilishwa 32, simu za kiganjani 98 na fedha kiasi cha Sh milioni 44 zilizokuwa zimeibwa

Pia, Katabazi amewataka wananchi mkoani humo kutoa taarifa polisi pindi wanapowatilia shaka watu au kikundi cha watu.

Amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuacha tabia ya kuwaamini wahalifu wanao walaghai kwa kupata nafuu ya riba wa mkopo au pembejeo mtandaoni kwani ni waongo na hutumia mwanya huo kujipatia kipato

Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara kupitia kitengo chake cha kuzuia wizi wa kimtandao linaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza ushiriki wao katika kuzuia na kubaini uhalifu.

Habari Zifananazo

Back to top button