Trafiki kutumia chipu, kamera kudhibiti bodaboda

JESHI la Polisi kitengo cha usalama barabarani linajipanga kuanza kutumia teknolojia ya kisasa kudhibiti madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda.

Mkuu wa usalama barabarani nchini, Ramadhan Ng’azi alisema Dar es Salaam kuwa  pia wana lengo la uhakiki ni kuthibitisha kama madereva wa magari binafsi na bodaboda wanamiliki leseni kwa kuzingatia utaratibu.

“Jeshi la Polisi linataka kuingia kwenye teknolojia ya kisasa ambapo kila bodaboda atasajiliwa na kupewa chipu maalumu na barabarani tutafunga kamera itakayopiga picha, na sisi kupitia mitambo yetu tutambua huyo dereva ni ya nani, anaishi wapi na ilikuwa inaendeshwa na nani kwa hiyo tunafikiri kupitia mifumo ya kisasa tunaweza kuwathibiti bodaboda,”alisema Kamanda Ng’azi.

Advertisement

Alisema kwa Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani limekuwa likihakiki leseni za madereva hasa madaraja ya C na E wanaoendesha malori na mabasi na sasa wanajipanga kuanza kuhakiki leseni za madereva wa magari binafsi na bodaboda.

“Zoezi la kuwakagua madereva wa magari binafsi linatarajiwa kuanza hivi karibuni  na upande wa bodaboda ni kundi ambalo linapasua kichwa na ni kundi ambalo tumejaribu kuwapa elimu sana lakini mabadiliko kwao ni madogo ndio maana kwa sasa tunatafuta mwarobaini wao,” alisema kamanda Ng’azi.

Kwa upande wa vyuo alisema kuna vyuo vimetengwa kutoa madaraja hayo mfano Chuo cha Usafirisha cha Taifa (NIT) Dar es Salaam, Veta Morogoro, Mbeya, Mtwara na Chuo cha Ufundi Arusha.

“Leseni za madaraja hazitolewi kwenye vyuo binafsi na wamezuiliwa kwa sababu hawana sifa endapo kuna chuo chochote kiliwadanganya madereva kwamba baada ya kusoma watapewa leseni kwa madaraja C na E kwa ajili ya kupasishwa kuendesha mabasi na malori hicho ni kinyume cha sheria kwa hiyo waende kwenye vyuo tajwa ili kuepuka usumbufu,” alisema kamanda Ng’azi.

Mwishoni mwa Februari mwaka huu Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Camilius Wambura alifuta Dawati la Leseni la Jeshi la Polisi baada ya kubaini kuna ukiukwaji wa maadili.

Baada ya uamuzi huo liliundwa dawati jipya la utoaji wa leseni  na baada ya kuunda dawati jipya kikosi kilitakiwa kuhakiki ni leseni zipi zilipatikana kiuwalali na zipi hazikufuata utaratibu pamoja na kujua dereva gani ni mahili katika eneo lake la kazi na madereva gani sio mahili.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *