Wakulima Mtama wajipanga kilimo biashara

WAKULIMA Wilaya ya Mtama mkoani Lindi wamejipanga kufanya kilimo biashara kupitia zao la mihogo ili kuinua uchumi wao na kuthibiti upungufu wa chakula.

Mpango huo umekuja baada ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) Kituo Cha Naliendele kufanya tathmini ya pamoja na wakulima hao kwenye mazao ya mihogo ambayo yametokana na aina nane za mbegu bora ambazo zimegunduliwa na Taasis hiyo na kuthibitishwa kuidhinishwa na Mamlaka ya kuthibiti ubora wa mbegu nchini.

Wakulima hao wamesema kupitia tathmini hiyo wamebaini uwepo wa mbegu ambazo wakitumia zitawasaidia kufanya kilimo biashara kupitia zao la mihogo mkoani humu.

Tathmini ilifanyika katika shamba darasa la TARI Naliendele katika Kata ya Kiwalala Wilaya ya Mtama.

“Tumefanya tathmini pamoja na wataalamu wa hizo mbegu bora, nimegundua ni nzuri sana, zinakuwa kwa wakati, zinazaa, sana nikizitumia zitanipa faida hasa kibiashara zaidi” amesema Sinde kirumbe Mkulima Wilaya ya Mtama.

Kirumbe pamoja na wakulima wengine wamekuwa wakifanya kilimo cha mihogo kwa kutumia mbegu za asili ambazo ni kushindwa kupata faida.

“Mimi ni mkulima wa Mihogo ambaye nilikuwa natumia mbegu tu za kienyeji ambazo hazinipi manufaa katika kilimo zaidi ya kupata chakula kidogo cha familia” amesema Bendita Mkanga Mkulima Mtama.

“Mbegu za asili hazizai sana, na lazima tulime kufuatisha msimu tu, zinakuwa na magonjwa mengi Sana,” amesema Aziza Nungu.

Mtafiti wa Mazao Jamii ya Mizizi ya Mihogo na Viazi Festo Masisila amesema mbegu za asili zinabiliwa na ugonjwa wa michirizi ya kahawia ambao unasababisha hasara mpaka asilimia 85 ya Mazao.

Ugonjwa mwingine ni Batobato Kali ambao pia unasababisha hasara ya Mazao asilimia 100.

“Tunasisitiza wakulima wazitumie hizi mbegu bora ambazo zimfanyiwa utafiti, mbegu zipo TARI na maeneo mengi hapa Kusini,” amesema.

Masisila amesema TARI Naliendele imezalisha zaidi ya mbegu bora nane kukuza kilimo Kanda ya Kusini. Mbegu hizo zina sifa nyingi nzuri ikiwemo kuzaa kwa wakati, kuzaa kwa kiwango kikubwa, kuhimili magonwa na ukame.

“Mbegu hizi zina sifa nyingi moja ya yake, zinazaa kwa wakati ndani ya miezi tisa mpaka 12 zinakuwa zimeshakomaa vizuri kabisa kwa matumizi ya aina yoyote,” amesema.

Mtafiti huyo amesema hizo bora huzaa tani 10 na zaidi kwenye hekari moja ikilinganishwa na za asili ambazo zinazaa kuanzia tani tatu kwenye hekari moja.

Habari Zifananazo

Back to top button