Mfumo wa anuani za makazi Mfumo wa anuani za makazi ufanikishaji wa sensa 2022

HATUA iliyofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) miaka 10 iliyopita ndio imetumika kufanikisha sensa ya watu na makazi mwaka 2022.

Kutokana na hatua hiyo, makarani na wasimamizi wa shughuli hii wamewezeshwa kufika kwenye kaya husika kwa urahisi.

Mwaka 2012, TCRA ilikamilisha mfumo wa anuani za makazi na postikodi na kuuchapisha katika Gazeti la Serikali namba 220 la tarehe 22 Juni mwaka huo. Ulikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa katika kuwapatia Watanzania anuani za uhakika.

Mfumo wa anuani za makazi na postikodi unaondoa kero na usumbufu wa kuelekeza mtu nyumbani kwako kwa kumwambia: Fuata barabara ya vumbi, kisha pinda kushoto baada ya kontena jekundu, kata kulia baada ya wanapofyatua matofali, kisha kushoto baada ya kibanda cha mkaa na utaona nyumba yenye paa la bluu mbele ya meza za mamalishe.Vitu hivyo vikihamishwa na watu hao wakihama itabidi kutoa maelekezo upya.

Mfumo wa anuani za makazi unatambua mtu anapoishi kwa namba ya nyumba na jina la barabara au mtaa. Mfano: Kimara Baruti, Barabara ya Sofia Kawawa, nyumba namba 24.

Pamoja na kurahisisha kufikiwa kwa maeneo mengi kwa ajili ya huduma mbalimbali, mfumo wa anuani za makazi unarahisisha kutambulika kwa nyumba na majengo; mambo ambayo ni muhimu kwenye kupanga na kusimamia mipango mahususi ya kutoa huduma kwa wananchi.

Mfumo huo pia unarahisisha utoaji wa huduma za dharura kama vile uokoaji na kukabiliana na maafa.

Hebu fikiria adha ya zimamoto au gari la huduma za wagonjwa (ambulensi) kufika makazi ya mtu aliyekuwa anaelekeza nyumbani kwake kwa kutumia vitu vinavyohamishika.

Mfumo unaongeza ufanisi katika usimamizi wa makazi ya watu na unarahisisha mawasiliano kati ya serikali na wananchi kwa malengo mbalimbali kama haya ya sensa. Ni mfumo ambao uzinduzi wake ulimhusisha Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Mwanamfalme wa Uingereza, Prince Charles.

Miaka 10 baadaye, Februari 8, 2022, Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan aliuongezea nguvu alipoitisha kikao mahususi cha watendaji wakuu wa serikali na wakuu wa mikoa jijini Dodoma na kuagiza kwamba mfumo wa kuweka majina ya utambuzi wa barabara na namba kwenye nyumba nchini kote ukamilike kabla ya sensa inayofanyika sasa (Agosti).

Mara nyingi Watanzania wanapotakiwa kujaza anuani zao kwenye fomu wanaweka anuani ya posta; na nyingi ni za taasisi.

Hii haina tija kubwa kwani nchi nzima ina masanduku ya posta ambayo hayafiki 200,000 na mengi hayatumiki, kutokana na mwelekeo wa kupungua kwa barua zinazopitia posta kutokana na maendeleo ya teknolojia ambayo yamewezesha kuwepo njia za mawasiliano rahisi na zenye ufanisi zaidi.

Rais Samia alielekeza kwamba mfumo wa anuani na makazi utekelezwe kama oparesheni ambayo aliita Oparesheni Anuani za Makazi.

Rais Samia Suluhu Hassan akishuhudia Makamu wa Rais Dk Philip Mpango akipokea kwa niaba yake bango la anuani ya makazi ya Ofisi ya Rais, Ikulu baada ya
kuzungumza katika Kikao Kazi cha wakuu wa mikoa kuhusu mfumo huo Februali, mwaka huu jijini Dodoma

Wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ziliagizwa kuutekeleza chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Utekelezaji wa oparesheni hiyo ulianza kwa kuunda programu tumizi ya mfumo kukusanya taarifa za baabara, mitaa, njia na makazi.

Vilevile kulifanyika mafunzo ya kuongeza uelewa wa viongozi ngazi za mikoa, halmashauri na serikali za mitaa kuhusu mfumo wa anuani za makazi na posta.

Kila halmashauri iliandaa mpango wa utekelezaji na kutoa majina ya barabara na mitaa na namba za nyumba.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anasema wizara ilitenga Sh bilioni 40 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kuendeleza uboreshaji wa mfumo huu.

Shughuli hizo ni pamoja na kuhakiki miundombinu iliyowekwa wakati wa ‘Oparesheni Anuani za Makazi’ ili kuhakikisha kuwa viwango vimezingatiwa.

Nape anasema kumekuwepo malalamiko ya wadau kuhusu ubora wa nguzo zilizowekwa kwenye barabara na mitaa, sarufi ya majina yaliyowekwa na mahali nguzo ziliposimikwa. Haya na mengine yaliyojitokeza anasema yatarekebishwa.

Anasema wizara pia itahakiki taarifa zilizokusanywa kwenye oparesheni hiyo, itaboresha kanzidata na programu tumizi ya mfumo na itaendelea kuunganisha mfumo huu na mifumo mingine ya kutoa huduma za kijamii na kwamba kompyuta mbili zenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi data zitanunuliwa.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni kutoa elimu kwa umma, makundi maalumu ya kijamii kuhusu manufaa na matumizi sahihi ya mfumo na kujengea uwezo taasisi za umma na binafsi kutoa huduma kupitia mfumo. Anasema sheria ndogo zitatungwa kuwezesha ujenzi na matumizi ya mfumo.

Waziri anasema Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) itapitiwa upya pamoja na kanuni zake ili kuleta ufanisi katika matumizi ya mfumo wa anuani na makazi.

Shughuli nyingine zitakazofanyika inaelezwa ni kuandaa mwongozo wa namna mpya ya wananchi kufanya biashara kwa kutumia mfumo.

Inaelezwa kwamba mkakati wa usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa mfumo utawekwa. Aidha, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wake pia vitafanyika.

Mfumo wa anuani za makazi unaenda sambamba na mfumo postikodi, ambazo zinajulikana pia kama simbo za posta.

Huu ni mfumo maalumu wa alama, tarakimu na herufi inayotambulisha eneo au mahali mtu anapoishi au kufanyia shughuli zake.

Tanzania inatumia mfumo wa namba na herufi ambao una tarakimu tano. Namba zote tano zinaonesha kata; wilaya, mkoa na kanda.

Postikodi za sehemu yoyote Tanzania zinaweza kupatikana kupitia simu ya mkononi, kwa kutumia menu kwenye simu. Bofya 15200# na fuata maelekezo. Pia zinapatikana kwenye tovuti ya: www.tanzaniapostcode.com.

Anuani za makazi na mfumo wa postikodi ni muhimu katika uchumi wa kidijiti, hasa kwenye biashara mtandao na ufikishaji wa huduma za kielektroniki.

Mifumo hii itakuwa kitovu cha utoaji wa huduma za biashara mtandao, ambalo ni mojawapo ya lengo la mradi wa Tanzania ya kidijiti.

Kwenye hili, Tanzania inatakiwa kuonesha njia; kwani nchi yetu inaongoza Kamati ya Huduma za Posta na Biashara Mtandao ya Umoja wa Posta Duniani, wenye makao yake makuu Berne, Uswisi.

Habari Zifananazo

Back to top button