Abdulla azungumzia heshima kwa watunza nyaraka

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema viongozi wa serikali, wakuu wa idara na taasisi wana wajibu wa kuwatunza na kuwaheshimu watunza kumbukumbu na nyaraka (TRAMPA) na makatibu mahsusi (TAPSEA) kwa kuwa ni kada muhimu katika kutunza siri za serikali.

Alibainisha hayo wakati wa mkutano wa kitaaluma wa Trampa na Tapsea uliofanyika Fumba, Zanzibar jana ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Abdulla alisema viongozi wanapaswa kuwatendea haki watunza kumbukumbu na nyaraka na makatibu mahsusi hao ili watimize wajibu wao vizuri kwa viongozi. “Kada hizi mbili ni muhimu sana, na naamini wameiva vizuri, kwa hiyo mwende mkazitunze na kama ambavyo mnaenda kuzitunza kumbukumbu, kwanza tunawajibu wa kuwatunza ninyi kabla ya ninyi kutunza hizi kumbukumbu.

“Niwaombe viongozi wote twende tukawatendee haki vijana wetu hawa, tukatimize wajibu wetu kwao, na wao naamini watatimiza wajibu wao kwetu,” alisema. Alibainisha kuwa amelisema hilo kwa kuwa vijana hao walikula kiapo mbele ya Rais Samia, hivyo kuna baadhi ya viongozi wanaweza kuwatengenezea ‘zengwe’ ili kuwaondoa kwenye nafasi zao kwa sababu tu hawakuwa tayari kutimiza matakwa yao.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, pamoja na mambo mengine alisema kada hizo mbili ni muhimu katika utumishi wa umma, hivyo viongozi hawanabudi kuwaheshimu kwa kuwa kada hizo ndizo zinazoshika uhai wa viongozi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haroun Ali Suleiman alisema yeye ndiye aliyeshauri uanzishwe utaratibu wa watumishi hao kula kiapo cha uaminifu kwa kuwa wanajua siri nyingi zikiwemo za wizara, idara na taasisi za serikali.

Mwenyekiti wa Trampa, Devotha Mrope alimweleza Rais Samia kuwa ni matamanio ya kila mtunza kumbukumbu kuwa na idara yao inayojitegemea kwenye taasisi zote za serikali kwa kuwa moja ya sababu zinazofanya siri za serikali kuvuja ni kutokana na kusimamiwa na watu ambao hawajasomea utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.

Naye Mwenyekiti wa Tapsea, Zuhura Maganga pamoja na mambo mengine, alisema baadhi ya waajiri huwanyima ruhusu watumishi wa kada hizo au kugoma kuwagharimia wanaposhiriki mikutano kama hiyo, hivyo akaiomba serikali iwasaidie katika hilo, hoja ambayo Rais Samia aliwaagiza mawaziri wenye dhamana kuifanyia kazi. Wanachama zaidi ya 8,000 wa Trampa na Tapsea walishiriki mafunzo hayo Zanzibar.

Habari Zifananazo

Back to top button