RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ataendelea kupanga safu za uongozi mbalimbali katika serikali ya awamu ya sita hadi pale mambo yatakapokaa vizuri kiutendaji.
Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa 16/6/2023 kwenye Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma kwenye hafla ya kuwaaapisha viongozi wateule wakiwemo mabalozi, naibu katibu wakuu na washauri wa masuala ya siasa.
Ameongeza kuwa sababu mojawapo ya kufanya uteuzi huo ni kutoridhishwa na utendaji wa awali katika baadhi ya sehemu na kuwataka walioapishwa leo kufanya kazi kwa bidii na weledi na ili kuongeza ufanisi zaidi katika nafasi wanazoenda kuzitumikia.
Viongozi walioapishwa leo kwa upande wa Naibu Makatibu wakuu ni Rogatus Hussein Matvilla ambaye ni Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais – TAMISEMI (Miundombinu) na Kamishna Benedict Wakulyamba ambae ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Rais Samia amemtaka Matvilla kusimamia vizuri fedha zinazopelekwa kwenye ujenzi wa miuondombinu inayosimamiwa na TAMISEMI ili iendane na thamani yake huku akimtaka Kamishna Wakulyamba kusimamia nidhamu ya Askari ambao wanahusika na ulinzi wa hifadhi zilizopo nchini.
Kwa upande wa washauri wa Rais ambao wanahusika na siasa na uhusiano wa jamii ni William Vangimembe Lukuvi Abdallah Bulembo, Balozi Rajab Omari Luhwavi, na Haji Omar Kheir ambao Rais Samia amewataka kwenda kuangalia mahusiano ya jamii na siasa na kuja na mapendekezo ambayo yatasaidia kuboresha hali iliyopo.
Na Mabalozi ni Pamoja na Dk Moses Mpogole Kusiluka, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Salim Othman msaidizi wa Rais anayeshughulikia masuala ya siasa na Dk Kassim Mohammed Khamis ambaye ni msaidizi wa Rais anayeshughulikia masuala ya hotuba.
Awali wakati wa uapisho huo Viongozi wa Kitaifa waliposimama kutoa nasaha zao kwa waapishwa, Makamu wa Rais Dk Phillip Mpango amewataka kushirikiana vyema na viongozi wengine katika maeneo watayoenda kufanyia kazi huku kwa upekee akiwataka mabalozi kutumia nafasi hizo kudumisha mahusiano ya kidiplomasia nchini huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa sambamba na kutoa pongezi kwa walioapishwa amewataka kuwajibika kwa uadilifu katika majukumu yao akiwaahidi kuwapa ushirikiano.