skauti wachangia damu hospitali ya amana

SKAUTI 200 wa Kiislam wamechangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana jijini Dar es Salaam ili kujazia upungufu uliopo wa chupa 300 kati ya 500 zinazohitajika kwa mwezi.

Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama hospitalini hapo, Theodory Kyara alisema hayo wakati wa utoaji damu huo uliofanyika katika hospitali hiyo.

Kyara alisema matumizi ya damu katika hospitali hiyo kwa mwezi ni chupa 500, kama hospitali imekuwa na akiba ya chupa 200 hivyo uhitaji uliopo ni chupa 300.

“Tunashukuru kwa skauti hawa kwani kufika kwao kunawezesha kuokoa wagonjwa ambao ni wamama wajawazito, watoto na wale waliopata ajali. Tunaomba na watanzania wengine wajitokeze ili kuokoa maisha ya ndugu zetu wenye uhitaji wa damu,” alisema.

Alisema chupa moja ya damu inasaidia kuokoa maisha ya watoto watatu hadi wane, hivyo tatizo la damu linapojitokeza hospitali wanakwenda maeneo mbalimbali kuomba damu hiyo, hospitali jirani Temeke na Muhimbili ama damu salama.

Msimamizi wa Kitengo cha Maabara cha damu salama katika hospitali hiyo, Salome Kihampa alitaja faida za watu wanaojitolea kutoa damu kuwa ni pamoja na kujua kundi la damu walilonalo, pia wanapata majibu ya vipimo walivyopimwa ikiwemo homa ya ini, kaswende ama ukimwi bila gharama yoyote.

Alisema kwa vijana kama hao wa skauti wamekuwa wakiwapa elimu ya kujua kuwa damu ina umuhimu kwa jamii.

Kwa upande wake Mratibu wa skauti hao Yasin Rashid alisema wamewiwa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watanzania, hivo wanatoa hamasa na watu wengine waweze kuchangia damu.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x