28,000 waliokosa mikopo wajazwa fedha

WANAFUNZI 28,000 wa elimu ya juu mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yao baada ya serikali kuongeza Sh bilioni 84 na kufanya kiasi chote ilichotoa kwa mwaka huu wa masomo kuwa Sh bilioni 654 kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru, wakati wa mkutano wake na wanahabari Dar es Salaam jana.

Badru alisema bajeti iliyokuwa imepitishwa na Bunge kwa mwaka huu ilikuwa Sh bilioni 570 kuwapangia mikopo wanafunzi wote takribani 177,000 wanaoendelea na wa mwaka wa kwanza.

Advertisement

Alisema kwa bajeti hiyo ya Sh bilioni 570 ingefanya idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanufaika wa mikopo kupungua kwa idadi ya wanafunzi 42,000, lakini baada ya mashauriano, serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ilisema wakati wa kipindi cha mapitio ya bajeti itakamilisha maombi ya nyongeza.

“Kwa hiyo serikali imekamilisha utaratibu wa maombi ya nyongeza ya fedha ya mikopo ili wale wanafunzi wa mwaka wa kwanza waongezeke na kufikia idadi ya wanafunzi wa mwaka uliotangulia ambao ni 70, 000,” alisema Badru.

Aliongeza, “Maana yake bajeti nzima itatoka shilingi bilioni 570 hadi shilingi bilioni 654, kama kiasi hicho kisingeozeka, wanafunzi takribani 28,000 wa mwaka wa kwanza wasingepangiwa mkopo.”

Kwa mujibu wa Badru, uamuzi huo wa serikali wa kuongeza Sh bilioni 84, umeifanya bodi hiyo kukamilisha kuwapangia mikopo wanafunzi hao 28,000 na taarifa zao zinasomeka vizuri kwenye akaunti walizotumia kuomba mkopo (SIPA).

Pia alisema taarifa za wanafunzi hao tayari wameshazifikisha kwenye vyuo husika kukamilisha usajili wao na utaratibu wa kukamilisha malipo ya fedha hizo unaendelea.

Badru alisema fedha ya robo ya kwanza ya mwaka ya wanafunzi hao 28,000 imeshapelekwa vyuo husika na kiasi cha fedha kilichotumika kuwapangia mkopo wanafunzi hao ni takribani Sh bilioni 84 zilizoongezeka.

“Mpaka leo, wanafunzi 68,460 wa mwaka wa kwanza wapya wameshapangiwa mikopo na wamelipwa fedha ya robo ya kwanza na lengo letu kufikia wanafunzi 71,000,” alieleza.

Kuhusu rufaa, alisema dirisha hilo lilifunguliwa kwa siku saba na lilijifunga rasmi juzi ambapo wanafunzi 32,777 waliwasilisha taarifa zao za rufaa.

Badru alisema bodi yake itazipitia rufaa hizo na ikifika Novemba 26, mwaka huu wale waliokidhi vigezo watapangiwa mkopo na hapo watakuwa wamefika mwisho wa msimu wa kupanga mkopo.

Alisema mpaka sasa jumla ya wanafunzi 166,438 wameshapangiwa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 424.5 na miongoni mwao, wanafunzi wa mwaka wa kwanza ni 68,460 na wanaoendelea na masomo ni 97,978.

1 comments

Comments are closed.