Mikataba ya bil 507/- yasainiwa mwendokasi

SERIKALI kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imesaini mikataba mitano, ikiwemo minne inayohusu kuanza kwa ujenzi wa miundombinu ya usafi ri wa haraka wa mabasi (BRT) awamu ya nne.

Mikataba hiyo ilisainiwa na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta na wawakilishi wa kampuni zilizoshinda zabuni za ujenzi wa miradi hiyo zikiwemo nne kutoka China.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo Mtendaji Mkuu Besta, alisema mikataba yote minne inayohusu BRT itagharimu takribani Sh bilioni 507 na mkataba mmoja wa ujenzi wa barabara ya Tamco – Vikawe – Mapinga kwa kiwango cha lami utagharimu kiasi cha Sh bilioni 17.89.

Advertisement

Akizungumzia miradi minne ya BRT ikiwemo mitatu ya awamu ya nne, alisema mkataba wa kwanza ni wa ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 13.5 kuanzia Maktaba ya Taifa mpaka Mwenge ikijumuisha kipande cha Barabara ya Sam Nujoma kutoka Mwenge mpaka Ubungo.

Alieleza kuwa mkataba huo pia unahusisha upanuzi wa daraja la Selander, ujenzi wa vituo vikuu viwili vya mabasi, vituo vya kawaida vya mabasi 20 na vituo mlisho 10 na utagharimu Sh bilioni 174.38 na ujenzi huo umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 18.

Mkataba mwingine alisema ni wa ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa kilometa 15.63 kuanzia Mwenge mpaka Tegeta na unahusisha upanuzi wa madaraja matatu, ujenzi wa vituo vikuu vya mabasi, vituo vya kawaida vya mabasi 19 na vituo mlisho vitano.

Besta alisema mradi huo utagharimu Sh bilioni 193.850 na ujenzi umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 18. Kuhusu mkataba wa tatu alisema ni wa ujenzi wa karakana mbili na kituo kikuu cha mabasi kimoja na utagharimu Sh bilioni 60.98 na ujenzi umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 18.

Aidha, mkataba wa nne alisema unahusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara na upanuzi wa sehemu ya barabara ya Ubungo hadi Kimara yenye urefu wa kilometa tano kutoka njia sita hadi njia nane. Alisema ujenzi wake utagharimu Sh bilioni 71.48 na umepangwa kukamilika katika muda wa miezi 18.

Alieleza kuwa miradi yote hiyo ya BRT awamu ya nne Dar es Salaam inatekelezwa kwa kugharamiwa na serikali ikishirikiana na Benki ya Dunia kupitia programu ya Dar es Salaam Urban Transport Project (DUTP).

Alisema miradi hiyo yote, itahusisha ujenzi wa miundombinu mingine kama karakana katika maeneo ya Mbuyuni na Simu 2000 zitakazokuwa na uwezo wa kuegesha mabasi 759, sehemu za matengenezo ya mabasi, sehemu ya kuoshea mabasi na sehemu za kujazia mafuta. Pia alisema kutakuwa na ujenzi wa njia maalumu za wapita kwa miguu pembezoni mwa njia za magari mchanganyiko, kuweka alama za usalama barabarani, taa za kuongozea magari na za barabarani na kuweka kamera.

Besta pia alizungumzia mkataba wa tano unaohusu ujenzi wa barabara ya Tamco – Vikawe hadi Mapinga kwa kiwango cha lami na sehemu ya Pangani hadi Mapinga kilometa 13.59. Alisema barabara yote hiyo ina jumla ya kilometa 22 na inaanzia katika Mji wa Kibaha hadi Mapinga wilayani Bagamoyo.

“Barabara hii ni kiungo muhimu kati ya barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro, Arusha na Tanga kupitia Bagamoyo,” alisema.

Besta alisema mradi huo utajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 17.8 na muda wa utekelezaji wake ni miezi 12. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alisema Mradi wa BRT wenye awamu sita ulibuniwa na serikali mwaka 2004 kwa lengo la kupunguza msongamano.

Alisema mpaka sasa awamu ya kwanza ya mradi huo inayoanzia katikati ya Jiji hadi Morocco na Kimara imekamilika, awamu ya pili inayoanzia katikati ya jiji hadi Mbagala na ya tatu inayoanzia katikati ya jiji hadi Gongolamboto ziko kwenye hatua ya ujenzi.

Alitaja awamu nyingine ambazo ni ya tano kutoka Ubungo hadi bandarini itakayojumuisha kipande cha barabara kutoka Segerea na sehemu ya Mbagala na ya sita itakuwa ni kutoka Morocco hadi Kawe na Mbagala hadi Vikindu.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alisema miradi hiyo ikikamilika itaondoa kero ya msongamano na foleni ya magari na hivyo kurahisisha shughuli za uzalishaji.

1 comments

Comments are closed.