MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) akichukua nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Haji Ambar Khamis amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na viongozi hao watakuwa kwenye nafasi hizo kwa mwaka mmoja. Profesa Lipumba na Khamis walichaguliwa Dar es Salaam katika Mkutano Mkuu wa TCD.
Mkutano huo pia ulijadili masuala ya utekelezaji wa mipango ya TCD kwa mwaka 2023/24 yakiwemo mabadiliko ya katiba ya kituo hicho na maandalizi ya kongamano la demokrasia linalotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Katiba hiyo ilibadilishwa kuendeleza demokrasia, kufanya siasa za uwazi zenye maridhiano na kukosoana kistaarabu kwa ujenzi wa nchi. Baada ya kukabidhiwa uongozi huo, Profesa Lipumba alisema atasimamia kuongeza maridhiano na ushirikiano kama alivyofanya Kinana.
“Malengo ni kuhakikisha Tanzania inasonga mbele katika ujenzi wa demokrasia ya kweli, inakuwa nchi tulivu na iwe chombo au nyenzo ya kujenga uchumi shirikishi, kazi ambayo ni ya Watanzania wote na sisi tunaendeleza kazi hiyo,” alisema.
Profesa Lipumba alisema atasimamia kujenga mazingira mazuri ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ili chaguzi hizo ziwe huru na za haki. Khamis alisema wameridhika na hali ya kisiasa ilivyo sasa nchini ikiwa ni pamoja na kuruhusiwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na maridhiano baina ya vyama.
“Kwa kauli moja tumekubaliana kwamba masuala ya zamani na ya sasa ni tofauti, sasa hivi tumefikia mahala pazuri na kuna mwanga mkubwa wa kuihuisha demokrasia yenye ukweli,” alisema.
TCD ina kanuni za kupokezana nafasi ya uenyekiti kwa kufuata mfuatano wa kialfabeti wa wanachama wake ambao ni CCM, ACT-Wazalendo, CUF na Chadema. Kwa sasa ilibidi Chadema washike nafasi hiyo kutoka kwa CCM lakini kwa kuwa hawakuwa wanahudhuria vikao vya TCD awali, CUF imepata fursa ya kukiongoza kituo hicho.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema awali waliacha kushiriki vikao vya TCD, ila sasa wanashiriki na kuna umuhimu wa wao kufanya hivyo kwa sababu ya siasa za maridhiano zinazoendelea nchini.
“Tumekubaliana Profesa Lipumba awe mwenyekiti na sisi tutakuja kushika nafasi hiyo raundi zinazofuata, ni jambo ambalo tumekubaliana kwa maridhiano mazuri kabisa,” alisema Mbowe. TCD inaundwa na vyama vyenye wabunge, wawakilishi ama madiwani. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) kinawakilisha vyama vingine vya siasa vilivyosajiliwa nchini visivyo na sifa hiyo.