SERIKALI imesema kwa kushirikiana na sekta binafsi inajenga Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mlima Kilimanjaro (MKICC) chenye uwezo wa kuchukua watu 3,000 kwa wakati mmoja ili Tanzania iwe kitovu cha utalii wa mikutano barani Afrika.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, ameandika kuwa kituo hicho kitakachokuwa na hoteli mbili za hadhi ya nyota tano zenye uwezo wa kulaza wageni 1,000 kwa wakati mmoja, kitajengwa Kijenge jijini Arusha.
Akiwa kwenye eneo hilo jana, Msigwa alisema mafanikio yoyote ya kiuchumi yanataka uwekezaji na kwa dunia ya leo lazima ushirikishe sekta binafsi ili mapato yanayokusanywa na serikali yatumike kutoa huduma kwa Watanzania.
“Kituo cha mikutano ni biashara sio huduma ya kijamii kwa hiyo sekta binafsi watakuja watawekeza na bahati nzuri serikali yetu imeunda chombo kinaitwa AICC (Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha), watasimamia hilo eneo…tunapokwenda kwenye uwekezaji mkubwa kama huu serikali inaangalia sana maslahi ya nchi yetu,” alisema Msigwa.
Akiwa na Msigwa katika eneo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Ephraim Mafuru alisema kituo hicho kina kiwanja cha ekari 90 chenye urefu wa kilometa mbili kutoka Mzunguko wa Barabara ya Impala hadi Kijenge itakapojengwa MKICC. “Dhamira ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Dk Samia Suluhu Hassan ya kufanya Tanzania kitovu cha utalii wa mikutano, ndoto hii itatekelezwa katika kiwanja hiki.
Tutaendelea kuwekeza katika kumbi kubwa za kisasa ili Tanzania iweze kushindana,” alisema Mafuru. Awali, Msigwa aliandika kuwa kituo hicho kitakachojulikana kwa Lugha ya Kiingereza Mount Kilimanjaro International Convention Center (MKICC), kitakuwa na kumbi sita ndogo kwa ajili ya mikutano.
“Hii ni safari muhimu ya kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa mikutano barani Afrika,” aliandika Msigwa na kubainisha kuwa kituo hicho pia kitakuwa na nyumba za kuishi.
Alieleza kuwa MKICC pia itakuwa na maduka makubwa, nyumba za kulala watu mashuhuri wakiwamo marais 15, maeneo ya burudani, maeneo ya kupumzika, bustani na eneo la maonesho lenye uwezo wa kuhudumia watu 10,000 kwa wakati mmoja.
Alipozungumza na wanahabari, alisema Rais Samia anautazama Mkoa wa Arusha kimkakati na serikali imeamua kuiimarisha AICC kwa kujenga kituo kikubwa zaidi, na inafanya hivyo ili kuongeza mapato ya sekta ya utalii kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 17 ya sasa.
Comments are closed.