Wananchi Buhigwe walia ukosefu wa huduma za afya

WANANCHI wa kijiji cha Kumbanga Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wamesema ukosefu wa zahanati katika kijiji chao unasababisha kero na shida inayowalazimu kusafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kupata huduma za afya.

Masikitiko na malalamiko ya wananchi hao  yametolewa mbele ya Mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru aliyefanya mkutano wa hadhara kwenye kijiji hicho sambamba na kueleza tatizo la ukosefu wa zahanati pia wamesema kuwa  hakuna huduma za kituo cha afya kwenye maeneo yao.

Advertisement

Cecilia Mpenda mkazi wa kijiji hicho alisema pamoja na huduma za kawaida changamoto kubwa ipo  kwa wajawazito hasa wanaokuwa na changamoto za uzazi ambao hulazimika kutumia kiasi cha Sh 40,000 hadi 60,000 kufuata huduma za matibabu kwenye kituo cha afya Matyazo Wilaya ya Kigoma ambako pia hulazima kulipa Sh  100,000 hadi 200,000 kwa wajawazito wanaokwenda kujifungua huko kwenye kituo cha afya cha kanisa.

Mwananchi mwingine wa kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Yohina Issaya alisema kuwa imewalazimu kuwa wanahama kijiji kwenda maeneo mengine karibu na huduma za hospitali wanapokaribia kujifungua kwani kuwepo kijijini hapo na kukutwa na uchungu ili kujifungua wajawazito wenye changamoto wamekuwa wakikataliwa kutibiwa kwenye zahanati hiyo ya kanisa.

Akizungumzia malalamiko hayo ya ujenzi wa zahanati kwenye kijiji hicho Mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru alisema kuwa ameshatoa maelekezo kwa uongozi wa kijiji na wananchi hao kuanza kukusanya mawe, mchanga na kuanza ujenzi wa boma la zahanati hiyo ili ifike hatua ambayo serikali itamalizia huduma ziweze kuanza lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.

“Nimesimamia kuomba fedha serikali kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho na shilingi milioni 50 imepitishwa kwenye bajeti ya mwaka huu lakini kijiji hawajafanya lolote kuanza ujenzi huo sambamba na ujenzi wa kituo cha afya ambacho kitajengwa kati kati ya kata ya Muhinda na Mbanga lakini pia  hakuna lolote lililofanyika hadi sasa,”alisema Mbunge huyo.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *