TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeanzisha huduma mpya, kufufua na kuimarisha zilizokuwapo, zikifanywa na wataalamu mabingwa nchini baada ya serikali kutoa zaidi ya Sh bilioni 4.5 kununua vifaatiba.
Akitaja huduma hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Abel Makubi amesema huduma hizo ni kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua ambayo wagonjwa 31 wameshafanyiwa upasuaji.
Profesa Makubi amesema gharama za tiba hiyo nchini ni Sh milioni nane hadi 16 na iwapo wagonjwa hao wataenda kufanyiwa matibabu hayo nje ya nchi gharama ni zaidi ya Sh milioni 40.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili, Profesa Makubi alisema matibabu mengine yaliyoanzishwa MOI ni ya maumivu sugu ya mgongo bila ya upasuaji na kuwa huduma hiyo ilianza kutolewa Mei mwaka huu, na hadi sasa wagonjwa 97 wametibiwa.
“Huduma hii ni mpya tumeianzisha Mei mwaka huu na gharama yake ni shilingi milioni moja ila ukienda nje ya nchi kupata tiba hii gharama yake ni hadi shilingi milioni tisa,” amesema Profesa Makubi.
Ameitaja huduma ya tiba iliyofufuliwa ni ya upasuaji marudio ya vipandikizi ambayo wagonjwa 57 wamefanyiwa kwa kurekebisha nyonga na magoti kwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji kati ya miaka 15 hadi 19 iliyopita.
“Huduma hizi ni mpya, zimeiwezesha taasisi kupunguza kero nyingi za ucheleweshaji wa matibabu na hata wagonjwa wengine kupata madhara ya kudumu, lakini pia zimepunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa nje ya nchi,” ameafanua Profesa Makubi.
Amesema kwa sasa magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu yanatibiwa nchini kwa asilimia 96 na asilimia nne za wagonjwa wanaobaki ndio hupewa fursa ya kwenda nje kutibiwa.
Aidha, matibabu ya upasuaji wa mifupa hufanywa nchini kwa asilimia 98 na asilimia mbili tu ya wagonjwa wenye matatizo hayo ndio huenda nje ya nchi kupata tiba hiyo.
Sambamba na maboresho hayo, MOI imeendelea kuimarisha huduma za uchunguzi wa kisasa ambako huduma za maabara ya upasuaji wa ubongo jumla ya wagonjwa 276 wamehudumiwa.
Gharama za huduma hiyo nchini ni Sh milioni tano hadi 10 na iwapo mgonjwa ataenda nje kutibiwa gharama ya huduma hiyo ni kati ya Sh milioni 30 hadi 60.
Eneo jingine lililoboreshwa kwa mujibu wa Profesa Makubi ni huduma za uchunguzi ambako serikali ilitoa Sh bilioni 4.4 kwa ajili ya ununuzi wa mashine mpya mbili za kisasa ikiwamo MRI na CT scan.
“Mashine hizi mbili zinakaribia kufungwa na hii itasaidia kuboresha huduma za vifaa hivyo kwani hivi sasa moja ikipata hitilafu nyingine inaendelea, wagonjwa hawatasubiri tena muda mrefu kungoja huduma, bali ugunduzi wa magonjwa utarahisishwa sasa,” alisema Profesa Makubi.
Mbali na hayo, alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya ndani na nje ya nchi kuboresha huduma za afya ikiwamo kupata nafasi za mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi wa taasisi kwa lengo la kuwajengea zaidi uwezo wa tiba bobezi.