DAR ES SALAAM: TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imesaini mkataba wa makubalino na Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, kuandaa na kuhuisha mitaala ya somo la Historia na kuandaa vitabu vya kiada na ziada.
Utiaji saini huo umefanyika leo Agosti 11, 2023 katika kituo hicho cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Adolf Mkenda na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Pindi Chana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkenda amesema katika kituo hicho cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kuna vitabu vingi muhimu lakini havipo katika maktaba zote nchini.
“Baadhi ya vitabu nimeviona hapa lakini ukivitafuta maktaba havipo, majuzuu yaliyoandikwa kuhusu harakati kupitia mradi wa Hashim Mbita, hayapo katika ‘booklet’ za maktaba zetu.”Amesema Mkenda na kuongeza
“Kuna kazi kubwa ya ujenzi wa maktaba ni jambo jema lakini hapo mlipofika mmalizie, mkarabati maktaba zilizopo fedha za maendeleo zinunulie vitabu, maktaba ni vitabu sio majengo, kuna Veta weka maktaba na vitabu, sekondari za kata weka maktaba na vitabu bila hivyo mtapoteza vizazi.
“Badala ya kudhani tunaenda kujenga maktaba kila mahali hapa nchi alafu ndio muweke vitabu mtapoteza kizazi, kazi kubwa ya serikali ni kununua vitabu na kuvisambaza; ….. “Hasa hivi ambavyo vinatukumbusha tulikuwa na nini kabla ya ukombozi, tusije tukasahau, tunasamehe lakini sio kusahau ili thamani ya ukombozi ifahamike, vitabu vyote visambazwe vijana wavisome, fedha zilizokuwa kwenye maktaba zisipungue, sio kwenda kununua misumari na matofali ziende kwenye vitabu.”Amesema
Nae, Balozi Chana akizungumza amesema mkataba uliosainiwa ni kuendeleza vitabu vya kiada na ziada ili watoto wafundishwe kwa kina na kuondoa kasumba sisi waafrika hatuna historia au ushahidi wa kishujaa tuliorisishwa, na kwamba makubaliano yaliyoingiwa yanakwenda kwenye utekelezaji.
“Kuna janga la kupotea kwa historia, maadili, uzalendo inatakiwa kudhibitiwa kabla ya kupotea kwa historia yetu tukufu kutokana na mmomonyoko wa maadili. Lazima kuwe na maadili, yapo mambo kama nchi ni lazima tuyakemee kwa nguvu zote kwa mujibu wa mila zetu, desturi na historia yetu, ndoa za jinsia moja no.
“Mwarubaini wake ni hiki kilichofanyika leo kuhakikisha mitaala na vitabu mbali mbali vya kufundishia shuleni vinaeleza historia ya Tanzania na mchango wake katika ukombozi wa Afrika, ili kila kijana ajioene fahari ya kuwa Mtanzania.
Nae, Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk Aneth Komba amesema makubalino yaliyosainiwa ni kushirikiana katika kuandaa vitabu vya kiada na ziada, kupitia machapisho kwa usahihi na kutoa mafunzo kwa walimu mashuleni na walimu tarajali ili wawe mahiri katika masomo ya historia na historia ya Tanzania.
Kwa upande wa Mratibu wa kituo hicho cha ukombozi: Boniface Kadili amesema wana maudhui ya kutosha kwa wanafunzi kufahamu na kujua mchango wa nchi yao kwenye mataifa mengine na kwamba kuna maeneo 250 ya ukombozi yamehifadhiwa.
Comments are closed.