Dk Gwajima alaani mauaji ya mke

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amelaani tukio la mauaji ya mkazi wa mtaa wa Mkoani mjini Geita, Amina Hassan (34) yaliyosababishwa na ugomvi wake na mumewe.

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Geita imeeleza kuwa usiku wa Agosti 30 mwaka huu Amina alishambuliwa na mume wake kwa kutumia kitu chenye ncha kali mwilini na kumsababishia majeraha na baadaye kifo ilipofika Septemba Mosi mwaka huu.

Akizungumuzia tukio hilo kwa njia ya simu juzi, Dk Gwajima alisema amewasiliana na mtoto pekee wa Amina  na kumpatia uhakika wa kuendelea na masomo yake hata baada ya tukio hilo, chini ya usimamizi wa ofisi ya Ustawi wa Jamii.

Advertisement

“Nasisitiza wanandoa kutumia huduma za ustawi wa jamii pale wanaposhindwa kuelewana kwa njia za kawaida, kwani namba za watoa huduma wa ustawi tumetangaza kwenye mtandao wa wizara .

“Nimeagiza maofisa ustawi Mkoa wa Geita wawe karibu na mtoto wa marehemu kwenye kipindi hiki kigumu ili kuhakikisha anavuka salama, ni imani yangu Jeshi la Polisi litamsaka mtuhumiwa ili aje ajibu tuhuma zake na haki itendeke,” alieleza Dk Gwajima.

Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji wa Geita, Cathbert Byabato alikiri kupokea maelekezo ya Dk Gwajima na kueleza tayari wameanza kuyafanyia kazi kwa kuonana na binti wa Amina na kumhakikishia usalama.

“Tunaamini kuwa linapotokea jambo kama hili mtoto anakuwa hajitambui au anakuwa hana ndugu wa kuweza kumfanyia jambo lolote au kuongozana naye. Yeye alisema ni mwanafunzi na anasoma kidato cha kwanza na yupo tayari kuendelea na masomo,” alisema.

Alisema Ofisi ya Ofisa Ustawi wa Halmashauri ya Mji wa Geita kwa ushirikiano na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita imepokea jukumu kuhahakikisha binti huyo anapata mwanasaikolojia wa kike atakayempatia tiba ya akili.

 

 

 

 

/* */