33% ya watumishi wa mahakama wapoteza kazi utovu wa nidhamu

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya utumishi wa mahakama amesema walipokea mashauri 99 ya masuala mbalimbali ya kinidhamu  ambapo asilimia 33 ya watumishi walifukuzwa kazi katika kipindi cha  miaka saba iliyopita.

Kauli hiyo ilitolewa jana katika mkutano wa wadau uliowashirikisha viongozi wa serikali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Tabora na wakuu wa wilaya zote za mkoa huo kilichofanyika mjini hapa.

Jaji Juma alisema kwamba kuanzia  Desemba 2015 hadi Desemba 2022, Tume imepokea mashauri yapatayo 99 yanayowahusu mahakimu kwenye masuala ya nidhamu ambayo yalitokea kwenye kamati mbalimbali.

Alisema kwamba watumishi wa mahakama asilimia 33 walifukuzwa kazi kati ya hao asilimia 38 walisimamishwa kwa manufaa ya umma, asilimia 13 walipewa onyo na asilimia 15 walirudishwa kazini.

Jaji Mkuu alisema kwamba takwimu hizo zimeonesha kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati hizo imeweza kuisaidia tume kuweza kutoa maamuzi yake.

Alibainisha kwamba viongozi wa kamati hizo za maadili wanasaidia kuiheshimisha mhimili wa mahakama baada ya kuonekana tuhuma za kimaadili kwa mfumo wa kuzishughulikia ambapo hakuna mtu yupo juu ya sheria.

“Viongozi mkizijua changamoto zinazoikabili mahakama mtakuwa na nafasi za kuwaeleza wananchi wenu na mtaweza kuzitatua ili waiamini mahakama zilizopo nchini kwetu,” alisema.

Alisema kwamba Mkoa wa Tabora ni mkubwa kutokana na kuwa na kilometa za mraba 72,150, ni kubwa zaidi ya nchi ya Rwanda na Burundi, hivyo majukumu ya utoaji haki katika mkoa huu ni makubwa na ni mazito kiutendaji.

Aliwaeleza viongozi hao kuwa ukiwa na eneo kubwa kama hilo ni lazima linakuwa na changamoto nyingi, ambapo wakati mwingine zinaweza kutafsiriwa kuwa ni utovu wa nidhamu kumbe hakimu anakuwa amezidiwa kutokana na umbali uliopo na kushindwa kufikisha huduma kwa muda mwafaka.

Habari Zifananazo

Back to top button