‘Makumbi ya mnazi yanafaa kutengenezea mapambo’

TEKNOLOJIA ya kuongeza thamani ya makumbi ya mnazi imewezesha kutengeneza kamba zinazotumia kupandia mwani, kuvulia pamoja na mapambo mbalimbali ya nyumbani.

Mbunifu na mtafiti kutoka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), Paul Kipati amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO kuhusu faida za makumbi hayo ya mnazi ambayo yanaonekana kama takataka.

Kipati amesema maeneo mengi ya Mikoa ya Pwani, Mtwara, Lindi, Kilwa, Tanga na Dar es Salaam hasa eneo la Kigamboni, kumekuwepo na takataka nyingi zinazotokana na nazi, lakini zingekusanywa zingeongeza thamani ya zao la minazi.

 

“Watu  wakishavuna nazi zao wanatoa ganda la nje wanachukua nazi ya ndani lile ganda la nje wanatupa. Lile sio takataka ukienda mikoani huko maeneo mengi ya mkoa wa Pwani yametapakaa kwa kiwango kikubwa cha makumbi hayo, mengine yanachomwa moto lakini hayaungui inakuwa ni changamoto kwenye mazingira.

“Kumbe haya mabaki ya mnazi yakichakatwa yanatoa nyuzi ambazo ni imara zinasokota kamba mbalimbali ni matumizi makubwa kwenye jamii, kwa mfano kamba za mnazi haziloi maji wala maji ya chumvi hayaathiri kamba hiyo,” amesema.

Amesema wakulima wa mwani wanatumia kamba hizo kupandia, pia wanaofuga samaki huzitumia kwenye vizimba baharini na kwenye maziwa mbalimbali.

Amesema makumbi hayo ya mnazi yanatoa mbolea kwa ajili ya bustani za mbogamboga, kutengeneza mapambo na shughuli nyingi mbalimbali.

 

Habari Zifananazo

Back to top button