337 ruksa kurudia mtihani kidato cha nne

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeruhusu wanafunzi 337 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne warudie kuufanya mwezi ujao.

Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda amesema wanafunzi hao watafanya mtihani pamoja na watahiniwa wa mtihani wa kidato cha sita kuanzia Mei 2 hadi Mei 22, mwaka huu.

Profesa Mkenda alisema Dodoma kuwa miongoni mwa wanafunzi hao 333 walifutiwa matokeo baada ya kubainika walifanya udanganyifu na wengine wanne waliandika matusi kwenye karatasi za majibu.

Advertisement

“Tunawapa chance (fursa) kama wakitaka wanaweza wakawasiliana na baraza (NECTA) ili waweze kufanya mtihani wa kidato cha nne. Mtihani huu utatolewa wakati wa mtihani wa kidato cha sita,” alisema.

Profesa Mkenda aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, kwa kuzingatia utaratibu huo gharama za mtihani zitakuwa ndogo kulinganisha na za kuusimamia peke yake kwa kuwa ungegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.

“Wasimamizi wa mtihani watakuwa walewale wa kidato cha sita lakini humo wanaweza wakaingia wanafunzi wanne, watano, sita kulingana na utaratibu utakaowekwa.

“Watafanya mtihani wa kidato cha nne, mtihani utafungwa utakuja kusahihishwa, kwa hiyo utatuondolea gharama za ziada nyingi sana za kusafirisha mtihani, za kusimamia mtihani na kadhalika,” alisema.

Pia alisema shule zote zilizohusika katika udanganyifu wa mitihani hiyo bado zipo chini ya uangalizi na uchunguzi hivyo utakapokamilika hawatasita kuzifutia usajili.

Profesa Mkenda alitoa tahadhari kuwa hawatamvumilia yeyote atakayejihusisha na udanganyifu katika mitihani ya kidato cha sita.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *