337 waliofutiwa mitihani kufanya na wa kidato cha sita

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza kuwa wanafunzi 337 waliofutiwa Mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE) mwaka jana watafanya mitihani hiyo na watahiniwa wa kidato cha sita kuanzia kesho.

Pia Katibu Mtendaji wa (NECTA), Dk Said Mohamed amesema NECTA imevifungia vituo viwili vya mitihani ambavyo ni Shule za Sekondari Thaqaaf iliyoko Mwanza na Twibhoki iliyoko Mara baada ya kubaini ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji mitihani ya CSEE mwaka jana.

Dk Mohamed aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa maandalizi ya mitihani hiyo ya marudio imekamilika na itakwisha Mei 15 mwaka huu.

Advertisement

Alisema uamuzi watahiniwa warudie mitihani umezingatia kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa waliofanya udanganyifu chanzo ni mipango iliyoratibiwa na vituo husika kwa kushirikisha wamiliki wa shule, wakuu wa shule na wasimamizi wa mitihani.

Dk Mohamed alisema NECTA imewasilisha taarifa ya waliohusika kufanikisha udanganyifu huo kwa mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

“Vituo vilivyobainika awali kuhusika katika udanganyifu huo na kutangazwa kufungiwa kuwa vituo vya mitihani ni Shule za Sekondari Cornelius na Andrew Faza Memorial zilizopo Dar es Salaam na Shule ya Sekondari Mnemonic Academy iliyopo Zanzibar,” alisema.

Dk Mohamed alisema pamoja na kufungia vituo hivyo, NECTA ilijiridhisha kwamba shule za sekondari Thaqaaf iliyoko Mwanza na Twibhoki iliyoko Mara zilifanya ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa mitihani.

“Baraza limefungia vituo hivi kwa mujibu wa kifungu cha 4(8) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016 hadi tutakapojiridhisha kuwa ni vituo salama kuendesha mtihani wa kitaifa,” alisema.

Pia Dk Mohamed alisema NECTA itaendelea kuthamini mchango wa uwekezaji wa wadau katika sekta ya elimu nchini na kwamba haitakuwa dhamira au sifa kufungia shule nyingi kuwa vituo vya mitihani.

Alisema itakapobainika kuwa shule inaacha kutekeleza majukumu ya msingi kutoka kituo cha kutoa elimu na kufundisha maadili mema na kugeuka kuwa kituo cha kufundisha udanganyifu kwa watoto na kufanya vitendo vya hujuma watachukua hatua za kijinai na kinidhamu.

Dk Mohamed alisema baraza limesimama imara kutekeleza sheria, kanuni, miongozo na taratibu za uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kama zilivyo.

“Nawaomba watahiniwa wote nchi nzima wasidanganyike wala kujaribu kufanya udanganyifu katika mitihani iwe kwa ridhaa yao binafsi au kwa kuwezeshwa na shule zao, tutachukua hatua stahiki ikiwemo kufuta mtihani na kufungia shule iliyoratibu uhalifu huo kiwa kituo cha mtihani,” alisema.