Abiria afa ndani ya KQ akitokea New York

UONGOZI wa Shirika la Ndege la Kenya (KQ) umethibitisha kifo cha abiria kilichotokea katika ndege ya shirika hilo namba KQ003 iliyokuwa inatoka katika Mji wa New York nchini Marekani kuelekea katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi wiki iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo hivi karibuni ilisema mmoja wa abiria wa ndege hiyo alikuwa mgonjwa na malengo ilikuwa akifika Nairobi akapatiwe matibabu lakini alizidiwa katikati ya safari na kulazimisha ndege kutua kwa dharura mjini Casablanca, Morocco kwa matibabu.

“Baada ya kufika katika Kiwanja cha Ndege cha Casablanca wahudumu wa afya wa kiwanja hicho walimkuta abiria huyo akiwa haonyeshi dalili yoyote ya kuwa hai na baada ya vipimo walithibitisha kuwa ameshafariki dunia,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Advertisement

Shirika hilo lilitoa taarifa ya kuomba msamaha wateja wake kutokana na tukio hilo na pia kutuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na wanafamilia wa marehemu kutokana na kifo hicho ambacho hakikutarajiwa.

“Tunatoa salamu zetu za dhati za rambirambi kwa familia ya marehemu pamoja na marafiki na pia tunaomba radhi kwa wageni wetu wapendwa kwa usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na tukio hili,” ilisema taarifa hiyo.