KAMPUNI ya Huduma za Meli (MSCL) imesema meli ya Mv Mwanza – Hapa Kazi ni kubwa kuliko zote katika Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Mtendaji Mkuu wa MSCL, Eric Hamissi alisema hayo Mwanza wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana.

“Hakuna meli kama hii Kenya, Uganda wala nchi nyingine na ina madaraja tofauti tofauti sita, kuna daraja linaloanzia economy, business mpaka VIP na zote zitakuwa za kisasa kabisa,” alisema Hamissi.

Alisema meli yenye urefu wa meta 92.6 na upana wa meta 17 itakuwa na uwezo wa kusafiri kwa saa saba kutoka Mwanza kwenda Bukoba. Alisema za sasa zinatumia saa saba hadi 12 kutoka Mwanza kwenda Bukoba na kwamba ujenzi wa meli hiyo umefikia asilimia 71.

Hamissi alisema injini mbili tayari zimewekwa kwenye meli hiyo zenye ukubwa wa Kw 2,380 kila moja, jenereta mbili zimewekwa za tahadhari zenye ukubwa wa Kv 800 kwa kila jenereta.

“Meli ya Mv Serengeti yenyewe ilikuwa inatumia saa hadi 14,” alisema na kuongeza kuwa meli hiyo pia itakuwa inasafiri kwenda Uganda katika bandari za Port Bell na Jinja na bandari ya Kisumu nchini Kenya na Kemondo ya Bukoba kwa Tanzania,” alisema.

Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inabainisha kuwa chama kinatambua fursa zilizopo katika uchumi wa rasilimali za maji zikiwamo bahari, mito na maziwa

na rasilimali zilizomo ndani yake. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, pamoja na mambo mengine, CCM kimeielekeza serikali kuimarisha mifumo ya kitaasisi ya kuratibu na kusimamia maendeleo ya uchumi wa rasilimali za maji.

Kwenye ukurasa wa 32 wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26, unabainisha kuwa serikali imejenga meli mbili za mizigo ambazo ni Mv Ruvuma na Mv Njombe zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja na nyingine ambayo ni Mv Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa.

Kwa mujibu wa mpango huo, katika Ziwa Victoria, meli za zamani ikiwamo Mv Victoria na Mv Butiama zilifanyiwa matengenezo na zinafanya kazi na meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ikiendelea kujengwa.

Hamissi alisema vijana 200 wa Kitanzania wamenufaika na mafunzo ya uchomeleaji wa meli kupitia mradi huo wa ujenzi wa meli na wamepata ujuzi katika ujenzi wa meli hiyo unaotumia teknolojia ya kisasa.

Alisema meli hiyo iliyojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 89 imebaki kuzinduliwa na kupakwa rangi na mwisho wa Oktoba mwaka huu itaingia kwenye maji.

“Hiyo ni hatua kubwa sana katika ujenzi wa meli,” alisema na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan akisema baada ya kuingia madarakani kasi ya ujenzi wa meli hiyo imekuwa kubwa na fedha zimekuwa zikitolewa kwa wakati na ile dhima ya kazi iendelee inaonekana dhahiri.

Alishukuru msukumo wa serikali ya CCM kuhakikisha inatatua tatizo la usafiri kwa njia ya maji na akasema meli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 20, makubwa matatu na magari madogo 20.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana alipongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kupitia MSCL kwa hatua waliyofikia kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo.

Kinana alisema hayo alipotembelea meli hiyo katika bandari ya Mwanza Kusini akiongozana na viongozi wa serikali na CCM Mkoa wa Mwanza.

Habari Zifananazo

Back to top button