38 mbaroni Arusha kwa tuhuma anuai

JESHI la Polisi Mkoani Arusha linawashikilia watuhumiwa 38 wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu akiwemo dereva aliyekutwa akisafirisha kilo 390 za mirungi kwa kuzipakia kwenye lori la mafuta.

Akitoa taarifa hiyo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti.

Alisema operesheni hiyo ilifanyika kuanzia Septemba 5 hadi Septemba 10, 2022 na iliongozwa na Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha kwa lengo la kukabiliana na uhalifu ambao umeanza kutishia amani mkoani hapa.

Kamanda Masejo alisema Septemba 10 mwaka huu majira ya  saa 12:30 asubuhi katika Kata ya Kikwe wilayani Arumeru, jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata Allen Kasamu (49) dereva na mkazi wa Suye Jijini Arusha akiwa anasafirisha mirungi yenye uzito wa kilo 390.75.

Alibainisha  kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akisafirisha mirungi kwa kutumia gari la kubebea mafuta.

Katika operesheni hiyo  jeshi hilo lilifanikiwa kukamata pikipiki 13 zilizokuwa zinatumika katika matukio ya uhalifu, gongo lita nane, bangi yenye uzito wa kilo 70 pamoja na kompyuta mpakato ( laptop)  tatu.

Kamanda  Masejo alisema hadi sasa Jeshi la Polisi mkoani humo bado linaendelea na upelelezi ikiwemo kuwahoji watuhumiwa hao na pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kutolewa maamuzi.

Katika hatua nyingine, Kamanda Masejo alisema kwa Mkoa wa Arusha wananchi wameanza kujitokeza kusalimisha silaha zao katika vituo vya polisi .

Alitoa rai kwa wamiliki wa silaha wanaomiliki  kinyume cha sheria kufika katika vituo vya Polisi ama ofisi za watendaji wa mitaa kusalimisha silaha hizo katika kipindi hiki ambacho serikali imetoa msamaha kwa ambao watasalimisha.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button