MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kumuita mkandarasi anayeunganisha umeme Newala Vijijini ili apewe onyo la mwisho kwa kusuasua kuunganisha umeme kwenye vijiji ambavyo vimesalia wilayani humu.
Abbas ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) huku akisema mkandarasi huyo ni kama ameota ‘pembe’ kwa sababu alishapewa onyo na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kusuasua kwenye utekelezaji wa mkataba wa kuunganisha umeme Newala.
“Yaani hawa watu ‘Mkandarasi’ ni kama kuota pembe, yamewaota mpaka yamepiga cross yanarudi chini, kwa sababu wamakuja hapa mpaka viongozi wa kitaifa, Waziri mkuu, na Waziri Mkuu alitaka kuwafutia mkataba,” amesema.
Abbas ametoa agizo hilo baada Mbunge wa Newala Vijijini, Maimuna Mtanda kulalamikia mkandarasi huyo kwa kuwa na kasi ndogo lakini pia kushindwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kumtaka huyo mkandarasi kuhakikisha vijini 25 vinaunganishiwa umeme ifikapo mwisho wa mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake mwezi Septamba 14 mwaka huu Wilaya ya Newala ambapo alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha vijiji 25 vinaunganishwa na umeme kufikia mwisho wa mwezi Septamba.
Sambamba na hilo, Majaliwa alimtaka Mkuu wa Mkoa Abbas kumsimamia mkandarasi huyo kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza agizo hilo na kama wakishindwa amtaarifu ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya mkandarasi huyo.
Akiongea katika kikao cha RCC, Mtanda alisema mpaka kufikia Octoba 5 mwaka huu ni vijiji 11 tu ambavyo mkandarasi huyo ameunganisha umeme.
“Ninapata mashaka sana, hata Waziri Mkuu aliagiza kwamba kufikia Septamba 30, vijiji ishirini viwe vimewashwa na akawapa wafanye kazi gani,” amesema.