Shirika la Elimu Kibaha, wadau waungana kuwanoa vijana

Shirika la Elimu Kibaha, wadau waungana kuwanoa vijana

PWANI, Kibaha Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kupitia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (Kibaha-FDC) kwa kushirikiana na Chuo cha Biashara Kibaha (Kibaha Institute of Business-KiB) kimeanza kutoa mafunzo ya ujuzi kupitia kozi za muda mfupi kwa vijana balehe wenye umri wa miaka 15-19.

Mafunzo haya yanatolewa chini ya mradi wa AHADI unaofadhiliwa na Serikali ya Canada (Global Affairs Canada) na kusimamiwa na World Vision.

Mradi unatekelezwa na taasisi mbalimbali ambazo ni Kibaha Institute of Business, Babawatoto, KIWOHEDE and Medecins du Monde (MdM).

Katika mradi huo, KiB inawawezesha vijana balehe katika masuala ya kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali, ushauri wa kibiashara, kuwaunganisha vijana na fursa za mitaji ya biashara na ajira na kuimarisha ushiriki wa vijana katika mijadala ya kisera.

Mafunzo ya muda mfupi yanayoendeshwa na Kibaha-FDC na KiB, yalifunguliwa rasmi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Anathe Nnko na kuhusisha vijana 46 kwa awamu ya kwanza huku asilimia zaidi 60 wakiwa ni wasichana.

Akifungua mafunzo hayo, Nnko alikishukuru chuo cha KiB na World Vision kwa kuchagua kushirikiana na Shirika la Elimu Kibaha kupitia Kibaha-FDC katika kutoa mafunzo ya muda mfupi katika fani za hotelia, ufundi magari, udereva, useremala, mapambo, ushonaji na ubunifu wa mitindo pamoja na urembo na ususi.

Nnko aliwapongeza vijana balehe wanaonufaika na mradi wa AHADI na kuwaasa kuzingatia mafunzo kwa vitendo ili kujiimarisha kiujuzi na hatimaye waweze kujiajiri na kuajiri watu wengine baada ya kumaliza mafunzo hayo. Vile vile, aliwahimiza vijana hao kuwa na nidhamu wakati wa mafunzo.

“Nidhamu ni sehemu ya mafanikio, nidhamu itawasaidia kokote mtakapokuwa, sisi tumejipanga kutoa mafunzo bora,” amesema Nnko.

Mratibu wa Mradi wa AHADI kutoka World Vision, Eveline Sanga amewataka wanufaika hao wa AHADI kuwa makini darasani ili mafunzo watakayoyapata yawasaidie kupata kipato ambacho hatimaye kitaboresha maisha yao jambo ambalo ndiyo lengo kuu la mradi.

Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo cha KiB, Prof Lemayon Melyoki alikishukuru Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (Kibaha-FDC) kwa kukubali kushirikiana na Chuo cha KiB katika suala zima la kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vitendo chini ya Mradi wa AHADI.

Amesema kuwa mafunzo hayo yatachangia kwa kiwango kikubwa kufikia malengo ya mradi hasa katika kujenga uwezo wa kiuchumi kwa vijana.

Pia, aliwaasa vijana wanufaika kujituma vizuri wakati wa mafunzo ili waweze kupata ujuzi waliokwenda kujifunza Kibaha-FDC.

Mwanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (Kibaha-FDC), Asha Njowoka aliwakaribisha wanufaika hao na kuwataka kuwa na ushirikiano wakati wa mafunzo hayo. Naye, mnufaika wa mradi wa AHADI, Rosemary Emily aliahidi kutoa ushirikiano kwa walimu na wanafunzi wa Kibaha- FDC wakati mafunzo hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button