TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), imeanza kutoa mafunzo ya mwaka mmoja kwa wataalmu wake, ambapo wagonjwa 40 watafanyiwa upasuaji wa kisasa wa kutoa damu iliyovuja katika ubongo na kuziba mishipa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi wa MOI ,Dk Respisius Boniface amesema wanapata ongezeko la wagonjwa waliopasuka mishipa ya damu kwenye ubongo na husababishwa na presha.
Ameeleza kuwa kwa wiki wanapata wagonjwa waliopasuka mishipa ya damu kichwani na damu kuvuja katika ubongo saba mpaka 10 na kwa mwaka 120 hadi 150.
“Kila siku wataalamu wanazungumza magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi na wanahamasisha kuzuia kubadili style ya maisha yanaleta shida.
“Tumeona pamoja na kuzuia tujipange kuwatibu na tumeanzisha mafunzo maalum, ili kusaidia nchi yetu tutakuwa tunafundisha na tumeanza na Prof Atanasi kutoka Ujerumani haya ni mafunzo endelevu,” amesema.
“Sasa tumeanza na wataalamu wa MOI halafu baadae tutaenda na madaktari wa hospitali nyingine na tutafanya kwa mwaka mmoja,”amesisitiza.
Dk Boniface amesema oparesheni hizo zina gharama ya Sh milioni nane hadi 12 na nje ya nchi Sh milioni 50 hadi 60 hivyo kwa kila mgonjwa kiasi cha Sh milioni 40 zimeokolewa.
“Presha zamani ilikuwa watu wazima miaka 55 hadi 60, lakini sasa tunapata vijana hadi miaka 35 kwa sababu ya mabadiliko ya maisha na endapo mgonjwa akichelewa ubongo unakufa hata akifanyiwa matibabu hawezi kurudi kwenye hali ya kawaida,”ameeleza.
Daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Nasforas Rutabasigwa amesema kuwa utaalamu unaongezeka, hivyo wanatarajia kufanyia wagonjwa 40 kwa mwaka na kwa awamu nne watawafanyia wagonjwa 10.