40,000 wasafiri kwa SGR siku 20

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema tangu Juni 14, mwaka huu Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesafi risha zaidi yaabiria 40,000 kwa treni ya reli ya kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

Profesa Mbarawa alisema hayo mjini Morogoro jana baada ya kuwasili akitumia treni hiyo kutoka Dar es Salaam kukagua utoaji wahuduma za usafiri huo.

“Tumetoka Dar es Salaam saa 12 asubuhi, tumefika Morogoro saa 1:49 (asubuhi), kwamba treni hii ni treni ya
kawaida, tumesimama vituo vinne na kila kituo tumetumia dakika mbili,” alisema.

Advertisement

Profesa Mbarawa alisema amepata taarifa kuwa siku za mwisho wa juma kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili treni hiyo inajaa na inakuwa shida kupata tiketi.

Alisema inaonesha baadhi ya wanaotumia usafiri huo wanatoka mikoa ya Dodoma, Mbeya, Iringa na wanaegesha magari yao eneo la kitu cha Morogoro wanakwenda Dar es Salaam.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/wananchi-wampongeza-samia-kuanza-safari-sgr/

Profesa Mbarawa alisema kutokana na ongezeko la abiria TRC wataanzisha usafiri za Morogoro hadi Dar es Salaam mara nne kwa siku tofauti na sasa huduma hiyo ni mara mbili kwa siku.

Alisema kutakuwa na treni ya haraka na treni ya kawaida kwa lengo la kuwarahisishia abiria kupata huduma bora kwa wakati na ifikapo Julai 25 wanatarajia kuanza usafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema wakati wakitoka Dar es Salaam hadi Morogoro jana asubuhi abiria wengi walionesha kufurahishwa.

Malima alisema ukisafiri kwa basi kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam inachukua saa nne lakini ukitumia
treni ya SGR inatumia takribani saa 1:50.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/latra-yatangaza-bei-daraja-la-kawaida-sgr/

Malima alisema, treni ya SGR imekuwa ikiwarahisishia wananchi mambo na kwa siku za mwisho wa
wiki ni vigumu kupata tiketi kama hukukata siku tatu kabla ya safari.

Alisema treni ya SGR imekuwa kiunganishi kwa watalii wakitumia usafiri huo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kuchukua usafiri wa mabasi madogo kwenda hifadhi za taifa Mikumi na Udzungwa.

“Ijumaa walishuka hapa kituo cha SGR Kihonda idadi kubwa watalii na kukodisha basi ndogo tatu kwenda Hifadhi ya Taifa Mikumi wametalii na kurudi hapa kupanda treni kurejea Dar es Salaam na hii ni mwanzo kwani huko mbele watalii watakuwa wengi,” alisema Malima.