Takukuru Arusha wabaini uvujaji wa pesa za TRA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Arusha (TAKUKURU) imebaini ufujaji wa kodi ya zuio ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya zaidi ya Sh bilioni 1 katika halmashauri tatu za Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na wanahabari habari leo Oktoba 31, 2023 Kaimu Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Zawadi Ngailo amesema taasisi hiyo imefanya uchambuzi wa mfumo wa ukataji na ukusanyaji kodi ya zuio katika ununuzi wa vifaa na huduma kwenye Halmashauri ya Jiji la Arusha ,Halmashauri ya Meru na Halmashauri ya Arusha kwa mwaka wa fedha wa 2022/23.

Kamanda Ngailo alisema kuwa katika uchambuzi huo ulibaini ufujaji wa jumla ya Sh bilioni 1 katika halmashauri zote tatu ambapo Halmashauri ya Jiji la Arusha uchambuzi huo ulibaini kuwa Sh bilioni 46.1 zililipwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha kama malipo ghafi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na huduma.

Alisema katika malipo hayo Sh bilioni 1.2 kilitakiwa kulipwa TRA ikiwa ni malipo ya kodi ya zuio, aidha kiasi cha Sh milioni 292.7 ndio zimelipwa TRA kama kodi ya zuio huku kiasi kilichobaki ambacho ni Sh milioni 926.8 bado hakijalipwa TRA hadi sasa wakati ni kinyume na taratibu.

Kamanda alisema katika Halmashauri ya Meru taasisi hiyo ilibaini kuwa Sh bilioni 4.8 zililipwa na halmashauri hiyo kama malipo ghafi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na huduma, ambapo kati ya hizo kiasi cha Sh milioni 94.9 kilitakiwa kulipwa TRA ikiwa ni malipo ya kodi ya zuio,aidha kiasi cha Sh milioni 94.9 ndio kimelipwa TRA na kiasi cha zaidi ya Sh milioni 79.9 bado hakijalipwa.

Alisema katika Halmashauri ya Arusha, Takukuru ilibaini kuwa zaidi ya Sh bilioni 3.5 zililipwa na Halmashauri ya Arusha kama malipo ghafi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na huduma, ambapo kati ya hizo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 125.3 kilitakiwa kulipwa TRA ikiwa ni malipo ya kodi ya zuio lakini ni kiasi cha shilingi milioni 35 ndiyo zililipwa TRA kama kodi ya zuio na zaidi ya Sh milioni 90.3 hakijalipwa hadi sasa na halmashauri hiyo.

Kamanda alisema kuwa hatua zilizochukuliwa na Takukuru baada ya vikao na wadau wa Halmashauri ya Arusha, Halmashauri ya Meru na TRA waliweka maazimio kuwa hatua ya kwanza ni kuziba mianya ya rushwa iliyobainika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kodi ya zuio ya kiasi cha Sh milioni 170.3 inawasilishwa TRA kabla au ifikapo Disemba 31 mwaka huu.

Alisema vikao zaidi vitafanyika Halmashauri ya Jiji la Arusha na wadau katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba mwaka huu kwa ajili ya kuwekeana mkakati ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika katika ukataji na ukusanyaji wa kodi ya zuio pamoja na kuhakikisha kuwa kodi ya zuio ya kiasi cha Sh milioni 926.8 inawasilishwa TRA kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Kamanda Ngailo alisema kuwa taasisi hiyo pekee yake haiwezi kufanya kazi ya kupambana na rushwa bali jitihada za ziada zinahitajika kwa ushirikiana na Wananchi katika kutekeleza hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button