JESHI la Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita limelalamikia kukithiri kwa taarifa za uongo zinazotolewa na Wananchi kupitia namba ya dharura ya 114 hali inayorudisha nyuma utendaji wa jeshi hilo.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Geita, Hamisi Dawa amebainisha hayo kwenye mahojiano maalum na HabariLeo ofisini kwake mjini Geita.
Dawa amesema wanotoa taarifa za uongo ni kikwazo kwani wanakwamisha watu wenye taarifa za kweli kushindwa kupata laini ya mawasiliano na hata kuilazimu zimamoto kutumia gharama zisizo za lazima
“Tunawaonya wananchi wasitumie hii namba vibaya, hii tabia inarudisha nyuma, maendeleo kwanza tunatumia gari la serikali, tunatumia mafuta, tunatumia raslimali kwenda pale kumbe tukio halipo.
“Wakati mwingine unaweza ukashangaa barabara zetu ni changamoto unafika mahali unakuta tukio ni la uongo harafu unapata taarifa za tukio la kweli.
“Kwa hiyo unatoka kule kwenye tukio la uongo unaenda kwenye tukio la kweli, wanasema watu tunachelewa.” Alisisitiza Kamanda Dawa.
Kamanda Dawa amebainisha kero nyingine inayowakwamisha zimamoto ni ucheleweshaji wa taarifa kwani mara nyingi watu wanapambana na moto wakiona umewashinda ndio wanapiga simu ya zimamoto.
“Kikubwa wakati tukio linaanza tupigie simu ili tuwahi kufika, kama umeudhibiti sawa, kama umekushinda tutashirikiana na wewe kuuzima huo moto.” Amesema.
Ametaja changamoto nyingine ni suala la ramani, ambapo wengi wanajenga pasipo kufuata ushauri wa jeshi la zimamoto jinsi ya kujiokoa na kuepuka majanga na ramani nyingi hazizingatii usalama.
Kamanda Dawa ameongeza kwa mwaka huu wa fedha kuanzia mwezi Julai 2023, Mwezi Julai kulikuwa na matukio 24, kati yake matukio ya moto yalikuwa 15 na matukio ya maokozi yalikuwa tisa.
Ameongeza kwa Mwezi Agosti 2023, matukio ya moto yalikuwa 19, kati yake matukio ya moto yalikuwa 12 huku matukio ya maokozi yakiwa ni saba.
Amesema kwa mwezi Septemba 2023 kulikuwa na matukio 12, matukio ya moto yakiwa manne na matukio 11 ya maokozi huku mwezi Oktoba matukio yalikuwa 19, matukio nane ya moto na matukio 11 ya matukio.
Comments are closed.