Wanawake Mtwara wahimizwa ushirikiano

WANAWAKE katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wametakiwa kushirikiana kuhakikisha maendeleo ya wanawake yanapatikana katika janja zote.

Kushirikiana kwa wanawake imeelezwa kuwa ni pamoja na kubeba jukumua kuwalea watoto wa kike na kuhakikisha wanakuwa na kutimiza ndoto zao.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Sixmund Lungu amesema wanawake hao wabebe jukumu la kuwalea watoto wa kike kwa kuhakikisha wanakuwa na kutimiza ndoto zao.

Maadhimisho hayo yamefanyika leo Machi 7, 2024 katika kata ya Mtawanya kwenye manispaa hiyo yanayoambatana na kauli mbiu isemayo “Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”

“Mkishirikiana kwa pamoja mnaweza kuchochea mabadiliko miongoni mwenu na kuhakikisha uwezeshaji wa mwanamke unapatikana katika nyanja zote,” amesema.

Nyanja hizo ikiwa ni pamoja na elimu, afya siasa, ajira, utamaduni na katika shughuli za kibiashara.

Aidha ushirikiano huo utawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba watoto wa kike ambazo ni kikwazo cha kutimiza ndoto zao ikiwemo mimba katika umri mdogo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii katika manispaa hiyo, Juliana Manyama amesema katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo manispaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha kusaidia watoto na wanawake la Rizex Foundation kwenye manispaa hiyo, Riziki Suleiman amewahimiza wanawake hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuinua familia zao.

“Kwa wale wanaopitia changamoto mbalimbali niwaombe kutokukata tamaa juu ya changamoto hizo, muendelee kumtanguliza Mungu katika kila jambo mnalolifanya,” amesema Suleiman.

Habari Zifananazo

Back to top button