Mikakati kukomesha ukatili yawekwa

Madawati, majukwaa kuazishwa shuleni, mfumo wa malezi kusukwa upya

MNAMO mwezi Juni na Julai ,2022 niliandika Habari na Makala zinazohusu ukatili kwa watoto nikiangazia zaidi shuleni.

Makala na habari hizo zilieleza ni jinsi gani ukatili kwa watoto unavyoangamiza taifa la kesho kimya kimya huku nikichambua masuala kadhaa yanayosababisha ukatili na nini kifanyike.

Niliandika jinsi mmoja wa watoto alivyoeleza ni njia gani muuza matunda aliyeko pembezoni mwa geti la shule alivyowalaghai na pia mmoja wa wazazi ambaye alibaini mtoto wake kufanyiwa ukatili huo baada ya kumdadisi.

Nilizungumza zaidi na wazazi wanne wa watoto ambao wamefanyiwa ukatili na walieleza ni namna gani walihakikisha mtuhumiwa anakamtwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Hadi sasa mtuhumiwapo ameshafikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kulawiti mtoto wa miaka nane huku mafaili mengine yakiwa bado hayajawasili.

MIKAKATI YAWEKWA KUKABILI UKATILI

Mara baada ya kuandika habari hiyo Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsi,Wanawake na Makundi Maalum katika bajeti yake ya mwaka 2022/2023 ya Sh bilioni 43.4 miongoni mwa vipaumbele nane ni kuandaa mpango kabambe wa kupambana na ukatili katika shule za Msingi na Sekondari .

Waziri wa wizara hiyo,Dk Doroth Gwajima anasema wizara kwa kutambua hilo inaanza mpango kababe Wakuanzisha Madawati ya Ulinzi na Usalama kwa watoto ndani na nje ya shule na pia Mabaraza yataanzishwa ili kuwashirikisha watoto katika kujadili masuala yanayowahusu.

Dk Gwajima anabainisha kuwa ili kufanikisha hili wizara imetenga kiasi cha Sh milioni 386.7.

”Vilevile, mtoto akiwa shuleni anatakiwa kupata fursa ya kushirikishwa katika masuala mbalimbali yanayohusu kitaaluma ikiwa pamoja na ulinzi dhidi yake ni suala muhimu sana Majukwaa hayo yataanzishwa katika ngazi za shule za Msingi na Sekondari,”anasisitiza.

Kuhusu vijana balehe kuanzia miaka 10 hadi 19 serikali imekusudia kutenga kiasi cha Sh Milioni 355.6 ili kusaidia changamto zinazowakabili kama maambukizi ya virusi vya UKIMWI, mimba za utotoni, ukatili ukijumuisha ukatili wa kimwili, kingono, Kisaikolojia, lishe duni, utoro shuleni kwa watoto wa kike na wa kiume na ujuzi duni unaoweza kuzifikia fursa za kiuchumi zilizopo.

Dk Gwajima anasema wanaratibu uanzishwaji wa Ajenda ya Kitaifa ya Uwekezaji katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe Nchini ya 2021/22- 2024/25 iliyojikita katika kukabiliana na changamoto zao.

Hapa anaeleza zaidi “Ajenda hii itaendelea kutekelezwa katika Mikoa 13 ya awali iliyopendekezwa kwa kuwa mikoa hiyo imeonekana kuwa na viashiria visivyoridhisha katika maeneo yanayowakabili makundi hayo.

Aidha anasema Wizara ilifanya mapitio ya awali ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na kuainisha mapungufu katika Sera hiyo yanayokwamisha utekelezaji wa vipaumbele vinavyowahusu watoto na kundi la vijana balehe.

Pia Wizara hiyo imepanga kufanya tathmini ya kina ili kubaini mapungufu na kuandaa sera mpya katika mwaka huu wa fedha.

“Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 pia imeonekana kuwa na mapungufu, hivyo Wizara imeanza jitihada za kupitia sambamba na sheria nyingine zinazomgusa mtoto ili kubaini mapungufu zaidi kwa ajili ya kuziboresha,”anafafanua.

Mpango wa Serikali pia ni kufanya Kampeni ya “Twende Pamoja, Ukatili Tanzania Sasa Basi” yenye lengo la kujenga uelewa kwa jamii kuhusu usawa wa kijinsia na kupinga ukatili dhidi ya wanawake na Watoto kiasi cha Sh 119.6 zimetengwa.

“Tathmini ya utekelezaji wa Mpangokazi wa Taifa wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA – 2017/18 – 2021/22) pamoja na kuandaa MTAKUWWA II inafanyika huku Kampeni kubwa ya jamii ya kupinga na kutokomeza ukatili inayoenda kwa jina la Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) tayari karibu 8000 wamejiunga,”anasisitiza.

UKATILI MITANDAONI

Pamoja na hayo Dk Gwajima anasema ukatili mpya dhidi ya watoto mitandaoni umeendelea kushika kasi na kuwa kipaumbele cha kufanyia kazi kwa mwaka 2022/23.

Anasema Katika kukabiliana na aina mpya ya Ukatili dhidi ya Watoto Mitandaoni unaosababishwa na kukua kwa maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Serikali imeunda kikosi kazi cha Taifa cha Ulinzi na Usalama wa Mtoto mtandaoni.

“Kikosi hiki kinalenga kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya ukatili wa mtandaoni na kuwasaidia kutumia vifaa vya kieletroniki kwa usahihi na usalama.

Anaeleza majukumu mengine ya kikosi hicho kuwa ni kuratibu wadau katika Serikali na Sekta Binafsi kuhuisha masuala ya ukatili dhidi ya watoto mtandaoni na utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.

“Vilevile, Serikali imeandaa machapisho/majarida ya kufundishia watoto, wazazi na walimu kuhusu ukatili wa watoto mtandaoni.

Dk Gwajima anasema wataimarisha utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu athari za ukatili na namna ya kukabiliana na wahalifu wa ukatili huo kwa kushirikisha jamii.

“Elimu itatolewa kwa njia mbalimbali zikiwemo vyombo vya habari, mikutano, makongamano na mijadala katika ngazi ya jamii.

ELIMU YA MALEZI,MAKUZI KUTOLEWA

Kutoka na kukosekana kwa elimu ya malezi na makuzi anasema kiasi cha Sh milioni 94.5 zimeelekezwa katika elimu kwa wazazi na walezi kujua wajibu wao katika malezi chanya ya watoto yanayolenga kumjali mtoto katika mahitaji yake, kumlinda mtoto dhidi ya ukatili na kuhimiza kuzungumza na mtoto ili kujua changamoto na maendeleo ya mtoto kwa ujumla.

“ Ili kuwafikia wazazi/walezi wengi zaidi, Wizara itatumia mfumo mpya wa utoaji wa elimu ya malezi kwa njia ya kieletroniki yaani (Parenting Education Application)uliozinduliwa mwezi Mei, 2022 katika kutoa elimu ya malezi chanya kwa watoto na familia.

Dk Gwajima anabainisha kuwa kwa kushirikiana na wadau wanaratibu uandaaji na utekeleza Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambayo imelenga kuwekeza kwenye maendeleo ya mwanadamu kwa kukuza malezi jumuishi yenye tija katika uchumi.

”Ili kuimarisha malezi ya watoto katika ngazi ya familia, Wizara iko kwenye kuratibu uanzishaji wavituo vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ambapo, kwa mwaka wa fedha 2021/22, Wizara imeanzisha vituo vya mfano vya malezi jumuishi 30 katika Mikoa ya Dodoma (20) na Dar essalaam(10),”anasisitiza Dk Gwajima.

Anaongeza “Katika vituo hivyo, 15 vimekamilika vyenye jumla ya watoto 883 wakike 467 na wakiume 426 na Katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 tunatarajia kufikia vituo 100 zaidi kwenye Mikoa 4.

AJENDA YA WAJIBU WA WAZAZI

Kutokana na mabadiliko katika nyanja za kiuchumi na kijamii kumeonekana kuwa na upungufu mkubwa katika kutoa huduma za malezi kwa watoto hapa nchini kwa kuwa Watoto wanakosa huduma muhimu za malezi.

Dk Gwajima anaeleza kuwa Kwa kutambua hilo wameandaa ajenda ya Taifa ya Wajibu wa Wazazi na Walezi katika Matunzo ya Watoto na Familia ambapo, kupitia ajenda hiyo wameandaa jumbe mahsusi za kuelimisha wazazi wote kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto.

“Ajenda hii imeandaliwa katika nguzo tatu ambazo moja ni Mjali Mtoto kwa kumpatia huduma zote za msingi, Mlinde Mtoto dhidi ya Ukatili na Wasiliana na Mtoto mara kwa mara ili kuwa huru kueleza changamoto za makuzi yake na maendeleo.

JE MIKAKATI HIYO ITAFANIKIWA?

HabariLeo ilifanya mahojiano na wadau wa masuala ya ukatili wa kijinsia kwa watoto ambapo walieleza nji jinsi gani hatua hiyo inaweza kusaidia kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto.

Michael Sungusia ni Mtaalamu wa Masuala ya Haki na Ulinzin wa Mtoto anabainisha kuwepo kwa madawati katika shule za Msingi na Sekondari itachangia kutoa zaidi taarifa ya vitendo vya kikatili kwa watoto vinavotokea maeneo mbalimbali kwasababu kuna sehemu ambazo taarifa za matukio yatasikizwa na hatua kuchukuliwa.

“Lakini kikubwa zaidi kinapaswa kufanyika ambacho kipo katika vipaumbele vya Wizara ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu ukatili kwa watoto lakini aina za ukatili na namna ya kuripoti,”anashauri Sungusia.

Anasema changamoto kubwa zaidi ni tafiti kuonesha wanaowafanyiwa watu ukatili ni watu wa karibu kama mjomba,baba,kaka na wengine lakini kupitia mabaraza,majukwaa na madawati mtoto akikosa mtu wa kumwambia ukatili aliofanyiwa nyumbani au ndani ya jamii ataenda kusema shuleni.

Sungusia anasema pia mfumo wa malezi jumuishi ni muhimu kwa zamani jamii iliiishi katika misingi hiyo.

“kutoa elimu kwa vipeperushi ni njia bora na kushirikisha makundi yote sio suala la mwalimu tu.

Naye Katibu wa Kituo cha Kisarawe Orphanage Housev ,Florida John anasema hatua hiyo itafanya watoto kujiamini na kuweza kuzungumza mambo yananayowahusu.

“Watawekeana viongozi na wale viongozi wataenda ngazi za juu hivyo ni hatua nzuri.

Kwa upande wake Fatuma Kamramba ambaye ni Meneja Huduma ya simu kwa watoto C-Sema Zanzibar anasema hatua hiyo ni kujenga miundombinu rafiki ya utoaji taarifa kwa watoto.

“Ukiangali mfumo kama polisi hatuwachukulii kama raia wenzetu ni watu ambao wanaogopwa kama mtu mzima unaogopa kwenda polisi vipi kuhusu mtoto?

” Pia watoto ambao wanakuwa na mabaraza utaona wanajiamin na wanasimamia haki zao na wanazijua ,wanajua ukatili unatokeaji unafanywa na nani na wapi wanaweza kutoa taarifa.

 

Habari Zifananazo

Back to top button