|Rais Samia atoa shilingi bilioni 160

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa akitoa maelezo kwa umma kuhusu maandalizi ya kuwapokea Wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani 2023.

RAIS Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 vitakavyoweza kupokea wanafunzi 400,000 wa Kidato cha Kwanza wanaotarajia kuanza masomo mwezi Januari, 2023 ambao ni zao la Elimumsingi bila ada.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa leo Septemba 28, 2022 jijini Dodoma wakati akitoa maelezo kwa umma kuhusu maandalizi ya kuwapokea Wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani 2023.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa akitoa maelezo kwa umma kuhusu maandalizi ya kuwapokea Wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani 2023.

Amesema fedha hizo tayari zimeingia kwenye akaunti za Shule za Sekondari 2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya Kidato cha Kwanza 2023 na kupokelewa kwenye Halmashauri zote 184, kulingana na upungufu uliowasilishwa na kila Halmashauri husika.

Advertisement

“Serikali katika mwaka wa fedha 2021/22, ilitoa jumla ya Shilingi Bilioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya za Kata 231 ambazo ziko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji na zinatarajia kupokea wanafunzi mwezi Januari, 2023. “Amesema

Bashungwa amefafanua kuwa kwa mwaka 2023 takribani wanafunzi 1,148,512 wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ambapo ni wale walioanza darasa la kwanza mwaka 2016, ambapo serikali ilianza utekelezaji sera ya Elimu msingi bila ada Disemba mwaka 2015.

“Kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza ilikuwa kubwa sana, kwa kulinganisha na miaka iliyotangulia;…. “Kwa muktadha huo, wanafunzi waliopo Darasa la Saba mwaka 2022, ndio zao la kwanza la matokeo ya Elimumsingi Bila Ada” Amesema

Aidha, Amewaagiza Wakuu wa Mikoa nchi nzima kuhakikisha ujenzi unakamilika ndani ya miezi  miwili na nusu  yaani siku 755 na halmashauri zitakazoshindwa kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya viongozi husika.

“Wakuu wa Mikoa wasimamieni Wakurugenzi  kufanya matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa, na wakumbushwe kufuata miongozo inayotolewa  juu ya fedha hizo, ili kupata thamani halisi ya fedha kwa miradi inayotekelezwa” amesisitiza Bashungwa.

Wakati huo, Amewataka Wakuu wa mikoa kufuatilia kwa ukaribu ukamilishaji wa ujenzi wa Shule mpya kupitia mradi wa SEQUIP zikamilike kabla, au ifikapo Oktoba 31, 2022 ili ziweze kusajiliwa na kupokea wanafunzi mwezi Januari, 2023.